![]()
Leo Jumamosi, tarehe Mbili, Septemba, Taifa Stars wameibwaga Uganda moja bila. Michuzi anatueleza namna Wabongo wanavyoonyesha moyo wa kuipenda timu yetu. Anamnukuu mjuaji historia wa nchi yetu Tanzania, Mbunge wa Kinondoni, Idi Azan, aliyesema mapenzi haya yanafanana na kipindi kile tuliposimama imara kumtoa nduli Idi Amin wa Uganda mwaka 1979-80. Na enzi hizo ndizo mara ya mwanzo na ya mwisho kwetu kuingia fainali ya Kombe la Afrika.
Nilikuwa nikiifikiria hoja. Nikaunganisha mambo kadhaa kichwani. Nikafurahia uongozi wa leo unavyojaribu kuunga mkono mpira na michezo. Michezo ni sehemu mahsusi ya utamaduni wa taifa. Huunganisha watu. Huleta sifa kwa nchi. Huleta fahari. Husaidia uchumi. Huleta jazba. Nikaunganisha kwamba kocha wa Taifa Stars leo, Marcio Maximo, anatoka Brazili. Lazima nayo imechangia. Maximo, maana yake ni (“Juu” au “Zaidi” au “Mwisho kabisa”, kwa Kireno) anatoka katika utamaduni unaosisitiza mapenzi haya haya aliyosema Michuzi katika blogu lake. Nikakumbuka mwaka 1994 nikiwa Brazili. Siku nchi hiyo ilipotwaa kombe la soka la dunia. Kila mtu anacheka. Muziki kila kona. Nyimbo. Ngoma za Samba. Baharini watu tele wanaogelea wanaimba, wamejichora chora marangi rangi nyusoni, wanakula nyama choma, wanakunywa madafu, bia, kokakola, juisi za machungwa na maembe. Ona picha nimo nimekaa na fulana ya rangi ya Rasta na suruali kijani, chini ya jamaa aliyeshika bendera ya Brazil eti wananiimbia “Afrikano! Afrikano! Curti Conosso” (njoo sheherekea nasi) wamefurahi mpaka wanajisahau…utadhani eti mi nimehusika. Fundisho ni hilo. Michezo na utamaduni huleta furaha kwa nchi. Watu wakiwa na furaha huyapa zaidi matumaini maisha yao…
Hili gumzo, lakini, halijaisha….