Mbio za Marathon zimekuwepo miaka mia moja sasa. Zilianzishwa na hawa hawa Waingereza walioweka idadi yake kuwa Maili 26 na yadi 385 mwaka 1908. Dunia nzima imechukua riadha hii na kuibadili kuwa kilometa lakini Waingereza bado hawajakubali mfumo wa metriki. Lakini pamoja na hayo mbio za Marathon za London zinasemekana kuwa bora na za kusisimua kushinda zote duniani leo. Kwanza kwa vile zinashirikisha wanariadha mashuhuri na pili wakimbiaji wa kawaida wasiozoea kukimbia. Mtu yeyote mradi awe na moyo anaweza kushiriki. Ipo migao ya walemavu wasiokuwa na miguu wanaotumia magari na mikono, watoto chini ya miaka 16 na ya kadamnasi, inayogawa washindi wa kike na kiume.
Halafu pia la muhimu ni ufadhili na wafadhili. Wakimbiaji huchukua nafasi kuomba, kupigania na kutangaza mahitaji ya shida mbalimbali za kijamii hususan maradhi. Toka mwaka 1996 mbio za London zinafadhiliwa na kampuni ya siagi iitwayo Flora.
Ndiyo maana kila mahali utaliona bango la Flora. Wakimbiaji pia hulivaa bango hilo. Mwaka huu mbio hizo zilizofanyika Jumapili tarehe 13 Aprili, zilishirikisha wakimbiaji zaidi ya 35,000 wakiwemo Wamasai toka Tanzania walioleta sifa sana. Wamasai hawa waliletwa na shirika la Kiingereza liitwalo Green Force.
Wamasai hawa Sita (Nguvu, Lengamai, Kesika, Ninna na Isaya (kiongozi wao), walikimbia kutafuta fedha kujenga mabomba ya maji katika kijiji chao. Walimudu kukimbia kwa muda wa masaa matano na dk 24 na kukusanya paundi 60, 000 ambazo ni fedha nyingi sana. Fedha hiyo itatumiwa kujenga vijiji mbalimbali sehemu wanayotoka. Hili ni moja ya mambo makubwa mbio za London za Marathon (au Flora Marathon ) zinaweza kufanya. Labda Wabongo wanaotafuta mitaji ya maana kama hii wanaweza kufikiria kushiriki mbio za mwaka ujao. Tembelea tovuti ifuatayo ujue la kufanya….
http://www.london-marathon-getkidsgoing.co.uk/.
Ni vigumu kueleza kila ya aina ya waliokuwepo lakini blogu hii itajaribu kiduchu.
Picha niliyopiga chini imenifurahisha sana. Inakumbusha umuhimu wa michezo katika jamii. Inakumbusha umaana wa watu kukutana. Namna michezo inavyotukutanisha bin Adam. Michezo na riadha ni sehemu mahsusi ya utamaduni. Vijana hawa kutoka Kenya walinifurahisha namna walivyokuwa na fahari kwa nchi yao licha ya machafuko yaliyotokea kule. Licha ya mauaji. Walimshuhudia Martin Lel akimalizia marathon kwa muda wa haraka sana masaa mawili na dakika tano. Toka kushoto, Sammy, Brenda, Dennis, Winnie, Kente na Edwin. Kente alisema hufanya rapu…
Mvua ilikuwa ikinyesha siku nzima: mvua kubwa iliyohitaji miavuli na makoti, mvua ya rasha rasha, mvua ya manyunyu; lakini hata hivyo haikuzuia watazamaji kuja kushangilia wakimbaji zaidi ya 35, 000. Watu na familia zao, watoto kwa wazee, kila aina ya mkazi mjini London ama alishiriki kushangilia, kutazama au kukimbia.
Wakimbiaji wakibeba mizigo yenye zawadi ndogo ndogo kama fulana baada ya kumaliza marathon.
Kulikuwepo watu wa kujitolea toka kila sehemu. Hapa chini ni vijana wa kutoa huduma ya usingaji (masaji) kwa wakimbiaji. Wengi kati ya washiriki 35,000 walilalamika maumivu ya musuli, magoti na mwili mzima kwa jumla. Wasingaji hawa pia walitangaza chama chao kinachosaidia tatizo la ugonjwa wa Alzheimer unaowasakama wazee waliovuka miaka 65. Husakama akili, kuleta usahaulifu, kushindwa kuongea na mengine mabaya zaidi. Kati ya watu maarufu wenye ugonjwa huu ni bondia Muhammad Ali.
Wakimbiaji mwisho mwisho…wa maili 26 na yadi 385.
Wakimbiaji walijifaragua kwa aina kadhaa wa kadhaa za madoido, mapambo na kofia. Chini ni Graham ambaye alisema katimiza miaka 42. Mkewe ndiye aliyetupiga picha.
Wakimbiaji wakimalizia mbio hizo…uwanja wa Green Park, karibu na makazi ya malkia… (Buckingham Palace)…
Wakenya waliokuja kushuhudia washindi. Toka kushoto : Meshack Biwott, H Kipchumba, Kiprono na Karen. Mmoja wao aliniambia ni vizuri kuona wanariadha wanakumbusha kuwa Kenya kuna mazuri zaidi ya mauaji na tafrani zilizosababishwa na uchaguzi mwanzo wa mwaka huu…
Chini.
Mbele ya sehemu ya kukimbia; wapiga picha wamejipanga wakiraruka na kurarua. Kumbuka wanariadha maarufu walishapita…baada ya masaa mawili; sasa ni akina yakhe waliojitahadi masaa matatu kuendelea.
Chini, Mabango ya Wakimbiaji. Baada ya mbio walikuwa na sehemu zao spesheli za kukutana na ndugu, marafiki na washabiki. Hizi ni mbio za kila aina ya mtu, mwanariadha na asiyekuwa mwanariadha, mkimbiaji wa kudamkia na mgonjwa, mlemavu na mzee, dada na mama, kijana na baba.











Picha nzuri sana Kaka Freddy!
Hivi sababu kubwa ya Uingereza kukataa mfumo wa metriki ni ubishi tu au ni nini?
Simon,
Swali zuri.
Zuri kwa vile wengi duniani tunatumia lugha ya Kiingereza na maneno kama “miles” bado ni sehemu mahsusi ya msamiati wake. Ingawa Kiingereza ni lugha inayokubalika na kutumika bila wasiwasi, historia yake ni ya ukoloni na utawala wa maguvu. Tumelazimishwa kuitumia. Kwa hiyo bado kuna mabaki mabaki ya haya maradhi, na hawa jamaa bado “wanalo hilo” jihisia.
Hapa Uingereza miaka mingi sasa umekuwepo ubishi mkubwa kati ya wanaopenda metriki na wasiopenda. Ingawa vyombo vya habari mara nyingi hutumia metriki, bado pia hapo hapo hutumia mfumo wa zamani kama unavyoona wakati wa mbio za marathon majuzi.
Waingereza wana ukaidi fulani kuhusu jadi na desturi na hupenda sana kutetea masuala yote ya kale. Mathalani kuhusu utawala wa mfalme na malkia utaona bado upo. Hapo hapo kuna ambao hawautaki.
Ukija miji kama London utaona mazingira na mandhari nyingi za kikale kama barabara nyembamba, majumba na kadhalika.
Kuna halafu, hili suala la kujiunga na shirikisho la Ulaya. Waingereza wengi bado hawapendi na ni kama wanataka kujitenga. Ukinzano uko kila mahali. Hapo hapo unaonyesha demokrasia ya Kizungu ilivyo hai. Ni kama kwetu Bongo kuna wanaotaka muungano na visiwani na wasiotaka ( hasa Waunguja wenyewe); wanaotaka Jumuiya ya Afrika na Mashariki na wasioutaka shauri ya sababu zao mbalimbali.
kaka habari,naomba utueleze kuhusu freemasons!Hawa jamaa wako vp?Pia ninawezaje kupata kitabu chako cha TWENDE ZETU ULAYA?