JJ Otieno akiwa kazini Brixton, London, 2007 (picha na F. Macha)
Kwa miaka lukuki Waafrika tumeonyeshwa ovyo ovyo sana katika runinga na vyombo vya habari duniani. Mtazamo ulioenea ni kuwa tunakufa njaa, tunapigana wenyewe kwa wenyewe na taswira iliyozoeleka ni ya watoto wenye mainzi machoni, wanawake wenye matiti yaliyoanguka wanaobeba magunia, kina baba wanaotembea miguu mitupu, majeshi na viongozi wenye vitambi wasiojali maslahi ya wananchi…Aghalabu… ndiyo sababu ya kuanzishwa Africans in London TV Uingereza, kujaribu kuachana na maono haya muflis…Bahati mbaya kama hutumii mtandao au iwapo kompyuta yako haina ”Media Player” si rahisi kuiona runinga hii. Kwa sasa bado ni runinga ya mtandaoni. Lakini haitakuwa hivyo muda mrefu…Africans in London TV (AILTV) imeanzishwa na Mkenya Joseph Adamson akishirikiana na baadhi ya wanamuziki Waafrika tunaoishi mjini hapa nikiwemo mwandishi wa blogu ya Kitoto.
AiLTV ilivyoanza ilikuwa hivi mwaka 2007…
Bwana JJ ( kama anavyojulikana) mwanamuziki, fundi mitambo na mwendeshaji mkuu anafafanua katika kurasa nne nzima za mahojiano na jarida la televisheni TV-BAY karibuni kuwa lengo letu kuu ni kuitumia teknolojia vyema. Kaeleza pia kwenye barua iliyotolewa na makao makuu ya runinga za mtandaoni mjini Brighton Uingereza yaani IPTV Chanell :
“…Vipindi vyote vya AILTV vitatengenezwa na watu wenye asili ya Kiafrika, kuhusu watu wenye asili ya Kiafrika, au kuonyesha maslahi na utamaduni wa watu wenye asili ya Kiafrika.”
Kutokana na juhudi zetu moja ya kampuni bab kubwa zinazotangaza urembo nchini Uingereza ”Brand Design Agency” (BDA) imeahidi kuisaidia AilTV inayofanya kazi bila pesa na kwa kujitolea bado, kusimama dede…
Hebu angalia baadhi ya vipindi hapa; uwe na subira kama picha zitakwama au pole pole kutegemea na kompyuta unayotumia:
Je unataka kutengeneza vipindi vya runinga? Je unayo sinema? Jaribu kufanikisha ndoto zako kwa kuwasiliana nasi. Tutumie video fupi (demo) isiyozidi dakika tano kuonyesha mfano. Tuko pamoja.
Tuwasiliane:
Simu: +44-7595 040-952
+44-7986375-992
Au
+44-7961 833040
Sasa nimeamini kuwa freddy macha wewe ni “MULTI PURPOSE” hongera sana kwa mambo yote unayoyafanya katika jamii na hasa unapojaribu kuwa mstari wa mbele katika kutetea maslahi ya waafrika…Tanzania inabahati kubwa kwakuwapata wazalendo kama nyinyi… Mungu akubariki na uendelee mpaka mwisho. Naamini bado una mambo mengi ya kuyafanikisha kwa aajili ya taifa lako lakini naamini UTAFANIKIWA. Kwani nia unayo, nguvu unayo na uwezo wa kuyafanikisha hayo unao, kwa sababu unaonekana ni mtu mwenye nidhamu mno.
Ningeomba watanzania wengine tuungane kumuunga mkono kaka yetu ili kujenga taifa letu….
Pongezi kwa mawazo yenye kutia moyo na kwa jitihada za kuimulika afrika katika mtazamo tofauti. Kwa kadiri ninavyosoma maelezo kwenye tovuti hii nina imani kuwa tuko pamoja. Fikira zako hazijatofautiana sana na zangu. Ninayo michezo kadha na mmoja wao huenda ukang’oa nanga kabla ya Disemba mwaka huu. Nahitaji usaidizi wa kimipango (logistics) kwani tayari fikira za mchezo wenye ziko kamili. Nimenukuu anuwani yangu hapo juu na iwapo utaweza kuwasiliana nami huenda tukaungana katika kufanikisha vipindi vya kiafrika. Nina hamu kubwa ya kuasisi vipindi thabiti vya kiswahili.
Ah, basi ndo hivyo, Rajab Birya….
Ninaloweza kusema juu juu na upesi kuhusu AILTV ni moja. Ikiwa unayo video demo fupi ya kama dakika 5-10 hivi…fupi lakini inayoonyesha sakamoto yako…tafadhali tutumie aidha kwa barua pepe … au nitumie SmS nitakujibu kwa anuani ya kuposti. Simu yangu ni +44-7961-833040.
Kuhusu hayo mengine; niandikie barua pepe tuendeleze soga. Mawazo yako ndo’ yanayotakiwa; ndivyo wenzetu Wahindi au Wabrazili wanavo’endelea kisinema…wanashirikiana. Sisi kila mtu anataka kufanya kitu chake halafu anaharibu kwa kuwa tunalipua (cheki “quality” ya sinema zinazotoka Bongo siku hizi…zinaendelea kuwa nzuri lakini hazifai kabisa kimataifa…)na mambo ya sinema na video hayataki haraka hata kidogo.
Mawasiliano:
kilimanjaro1967@hotmail.com