“ELIMU HAINA MWISHO…”
Methali ya Kiswahili
Nchi yetu ina utata.
Mheshimiwa Rais kachorwa vibaya mitandaoni; miezi kadhaa iliyopita akazomewa ilhali kachaguliwa kwa asilimia 80 ya kura; Rais wa zamani, bwana Mwinyi akapigwa kofi hadharani; ajali za mabasi zimezidi,uvutaji bangi (hasa miongoni mwa vijana) umefikia asilimia 90 sehemu fulani fulani; viongozi mafisadi mahakamani; utovu wa nidhamu unaiandama nchi yetu ya Tanzania.
Tumeshasikia Muziki wa Kizazi Kipya ; tunahitaji pia Mawazo ya Kizazi Kipya: Wachapa kazi wa Kizazi Kipya; wananchi wenye nidhamu na mwenendo utakaodumisha amani na maendeleo ya Tanzania.

…Tulitazame jarida jipya la Lucky, lililoanzishwa karibuni mjini Dar es Salaam.
Mhamasishaji Innocent Flugence Swai, (pichani) mwalimu wa kompyuta, mjasiriamali, msomi anayeamka saa kumi na moja kila siku alikuwa na haya machache…
FM:
Je magazeti yanawezaje kusaidia changamoto na maendeleo ya Mtanzania?
SWAI:
Ninaamini kwamba majarida kama Lucky! Yana uwezo wa kuleta mwamko. Ni rahisi sana kulaumu, kulaumiwa na kulaumiana. Lakini tunaweza kujenga mawazo mbadala…
FM:
Jarida lenu lina makala za mseto. Ipo inayowaasa wanawake kutovaa sidiria zisizofaa, pana mahojiano na msanii Mrisho Mpoto halafu makala ya elimu yenye picha zenye watoto wakiwa darasani. Mmegusia pia tatizo la Ma Albino. Makusudio ni nini hasa?
SWAI:
Tanzania ina matatizo mengi mno! Ni vigumu kwa ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia kugusa tatizo moja, ndiyo maana tunaweza kuwa na malengo tofauti tofauti huku tukigusa matatizo kadha wa kadha ili kila mtu na hitaji lake tofauti apokee kitu toka kwetu.

FM:
Lucky pia lina lugha mbili, yaani Kiswahili na Kiingereza. Mkondo huu umeanza sana kukua katika nyendo za majarida ya kisasa Bongo. Je ni muhimu?
SWAI:
Ni muhimu, ni muhimu sana, manake ni jamii ambayo bado hatuna nguvu ya kumudu hizi mbili tu. Pia tunawalenga watu toka nyanda zote za jamii; hivyo ni muhimu kuhakikisha kila mmoja, mdogo kwa mkubwa pasipo kujali elimu, rangi, kipato, au itikadi anahamasishwa na jarida letu.
JITAFUTIE NAKALA YAKO YA LUCKY; UTAJIFUNZA LUGHA; UTAPATA HOJA MPYA; IKIWEZEKANA UNAWEZA HATA KUWAANDIKIA.
“UJASIRIAMALI SI LAZIMA IWE KAZI YA MTU MMOJA AU WAWILI, BALI KUNA WAKATI AMBAO KUNDI LA WAJISIRIAMALI HUJIUNGA PAMOJA NA KUANZISHA KAMPUNI MOJA YENYE NIA MOJA.”
-Dk Imani Kyaruzi, Profesa Msaidizi Chuo Kikuu cha London Graduate School of Management.
“KIPIMO CHA THAMANI YA MWANADAMU NI KIASI CHA FURAHA ALIYONAYO. AKIENDELEA FURAHA YAKE PIA HUWA KUBWA.”
-Bruce Lee, Mwigizaji sinema, Mpiganaji Gung Fu, Mwanafasalfa, 1963.
Mambo yanakua moto moto siku hizi kwenye blogu yako Macha na ndio maana nimekua napitia mara kwa mara kuangalia nini kipya umetuandalia wasomaji…
hili gazeti la lucky je limeanza lini? na sisi tulio huku ughaibuni tunaweza kulipata kwa njia gani?
Nash’kuru Vicky Majonje.
Kusema kweli ninavyojua jarida la “Lucky” ndio linaanza. Nimeelezwa litakuwa mtandaoni – online- karibuni…. kwa walio nje kama yalivyo magazeti mengine ya Bongo. Ila waweza pia kuwasiliana moja kwa moja na mhusika akakujibu:
innocent103@gmail.com