Karibuni nimeingia tena Bongo baada ya miaka miwili. Ama kweli kwa tunaoishi ughaibuni kurudi nyumbani ni kama kwenda hospitali. Kabla ya tiba lakini, shurti kuujua ugonjwa.

Tiba ya kwanza utani, masihara na vicheko. Hapa tuko Nyumba ya Sanaa (iliyofunguliwa na Mwalimu Nyerere mwaka 1983); leo imegeuzwa Jumba La Kila Kitu : baa, kamari, michezo, hoteli, mahali pa watalii kununua vito vya Tanzania, makutano kwa walioko mjini; kuchaji simu za mkononi, kutazama mpira mathalan ligi za Ulaya; sehemu ya kufanyia mazoezi na maonyesho.
Niko na Al Watan, baada ya kuchapa nyama choma kwa ndizi choma na vinywaji. Kwanza kabisa ni Innocent Swai mhamasishaji, mjasiriamali na mwendeshaji wa jarida jipya la “Lucky”; kushoto kwangu ni Issa Michuzi mpiga picha na mwanablogu maarufu siku hizi. (Picha na Blandina Kilama)
….Tiba ya kwanza ukirudi nyumbani ni vicheko. Unafurahia usiowaona muda mrefu. Swali la kwanza: je, utacheka muda gani?

Barabara itokayo Magomeni kwenda Ilala; hapa kuna mfano mzuri wa jiji la Dar leo. Magari makubwa makubwa aina zote : Pajero, Prado, nk. Barabara zilizopanuliwa; mioshi ya magari na vumbi; hapo hapo huyu bwana mgongo wazi akivuta mkokoteni (kwa baiskeli) akitafuta ajira. Mbio za mapanya zimeingia Bongo kiasi wahisi kila kitu mwendo mkali…
(picha ya mdau wa Kitoto)