
Zoezi maalum la kusaidia mabega kutokana na kazi mbalimbali zinazoathiri migongo, shingo na kichwa. Kuning’iniza bega moja ukizungusha mkono pande zote, huku mkono mwingine umeshika kiti au meza.
Semina zilitayarishwa na jarida la LUCKY linaloendeshwa kwa ushirikiano wa wananchi wanaojitolea mhanga kuelemisha na kuendeleza jamii ya Tanzania. Waliosimamia kazi hii ni Innocent Swai na mhariri wake Anna Rugaba. Zilifanyika Ukumbi wa British Council, Shule ya Sekondari Mwandege, Pwani; Nyumba ya Sanaa na Soma Cafe, Mikocheni.
Nilialikwa kuendesha mada nne muhimu:
1-Maisha ya Ughaibuni : utamaduni, elimu, kazi, uzoefu nk.
2-Afya, Chakula na Mazoezi ya mwili na viungo kwa jumla
3-Uandishi, fasihi na umuhimu wa kusoma na vitabu
4-Muziki : utunzi, uimbaji, upangaji na sanaa
5-Kitabu changu “Mpe Maneno Yake”

Mazoezi ya viungo, Ukumbi wa Vijana wa Tayoa (Tanzania Youth Alliance) Nyumba ya Sanaa.



Zoezi la kunyoosha mwili linalotokana na mfumo wa Yoga unaolinganisha kiwiliwili na mti (Tree Pose). Manufaa yake ni kukupa mwili usiojipinda ili kupunguza maumivu ya mgongo, kiuno na mabega. Pia husaidia akili , moyo na ari.
Wanafunzi waliojaa hamasa Shule ya Sekondari Mwandege, baada ya semina waliyovumilia saa tatu nzima. Mseto wa muziki, fasihi, rapu, mazoezi nk. (Picha na H. Macha)

Washiriki mada ya Maisha Ughaibuni, ukumbi wa British Council, wakiandika hoja. Maswali na majadiliano yalikuwa mengi. (Picha na Innocent Swai)

Mazoezi ya shingo Shule ya sekondari Mwandege yenye vidato vinne (Picha na H. Macha)
Anna Rugaba wa Lucky Magazine -Ideas for Living - lililotayarisha warsha hizi akisaidia washiriki kutoa maoni na mrejesho nyuma. (Picha na Innocent Swai)
Washiriki Soma Cafe : Asha Mtwangi wa Futures Group (www. futuresgroup.com) linalohamasisha vijana, afya na tamthiliya akiwa na Shanande Mushi…

Mshiriki na mtayarishaji Anna Rugaba wa Lucky akijaribu zoezi la kujinyoosha la Yoga mtindo wa Paka (Cat pose) ambalo husaidia viungo vingi ukiwemo mgongo, tumbo, miguu, mikono, mabega, mapigo ya moyo, kizazi na akili.
Waliohudhuria semina Soma Cafe ambapo suala la kusoma vitabu linafanyiwa kazi na kampuni ya E & D Limited pale Mikocheni. Kushoto ni Asha Mtwangi na kulia ni mwandishi chipukizi, Shanande Mushi.
Innocent Swai wa Lucky Magazine- Ideas for Living- akiwa na viongozi wahamasishaji wa Tayoa (Tanzania Youth Alliance) wanaosaidia magonjwa ya zinaa katika Nyumba ya Sanaa. Hawa walitukaribisha kwa mikono yote wakatupa ukumbi bure siku tatu. Katikati ni Meneja Mawasiliano, Benedicto Luvanda, mchapa kazi aliyehakikisha shughul hii inafanikiwa toka mwanzo hadi mwisho.

Kati ya wanafasihi wenye uzoefu mkubwa nchini ni Profesa Muyagbuso Mulokozi aliyehudhuria semina ya Soma Cafe. Baada ya kuwaeleza vijana kuwa mtaalamu huyu alikuwa kati ya wahamasishaji wangu wakubwa nikiwa naanza kuandika miaka ya Sabini baadhi walikaa wakimsikiliza. Hapa Prof Mulokozi anatoa store kuhusu gwiji wa fasihi ya Kiswahili Shaaban Robert.

Mwanamuziki mkongwe, Ibrahim Boss, aliyekuwa zamani mpiga ngoma (kit drums) bendi ya Revolutions (Kilimanjaro Hotel) miaka ya 80 alikuwepo Soma Cafe. Alisaidia pia kuchangamsha ngoma wakati nikitumbuiza kwa gitaa na nyimbo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Mwandege Boys, Bw. Enock Walter na baadhi ya wanafunzi viongozi. Shule hii isiyotumia kengele ni kati ya shule za kipekee nchini zinazotoa elimu inayowatayarisha wanafunzi kuwa makini zaidi kinidhamu, kitabia na kiakili.

Nyumba ya Sanaa…

Muziki wa gitaa, mashairi na fasihi

Majadiliano kuhusu fasihi, maisha ughaibuni, afya; maswali na majibu: Nyumba ya Sanaa…
Nimevutiwa na taarifa hii na vielelezo. Taarifa za awali za shughuli hizi tulizipata kwenye blogu mbali mbali, lakini hapa zimetolewa kwa upana na undani zaidi. Mambo ya aina hii ndio yanayotakiwa, ili kutoa mwelekeo muafaka kwa vijana wetu na wengine kwa ujumla. Nakutakia mafanikio zaidi na kila la heri.
Kaka Fredy, Salaam na Hongera kwa kazi.
Nilihudhuria semina siku mbili pale Nyumba ya Sanaa. Siku ya pili nilikuja na watoto wangu wawili wavulana Viheri na Shaposhi. Mambo makubwa mawili yalinifurahisha sana.
1. Elimu ya afya kuhusu mazoezi ya viungo na
2. Matumizi ya lugha.
Si kwamba vilikuwa vigeni sana lakini nilifurahishwa na upana wa uelewa wako kuhusu eneo hilo na kwa watoto wangu imewafungulia ukurasa mpya katika ufahamu wao na kila siku wanauliza namna wanavyoweza kuyafahamu kwa kina yale yote. Nina kazi ya kutafuta machapisho wayasome.
Kuhusu lugha hasa kiswahili. Kaka, ninavyokufahamu wewe ni kwamba umeishi nchi nyingi duniani na unajua lugha nyingi, lakini nilifurahishwa sana sana na jinsi ulivyokuwa unatumia kiswahili bila kuchanganya. Natamani kiwango chako cha elimu. Kwa kiwango hiki naamini kuwa unakithamini kiswahili na kukipenda. Ni kweli kuwa unapaswa kukipenda kwa sababu ni mzalendo. Hii ni tofauti sana na sisi wengi ambao tunafikiri kuonyesha kuwa unaelimika ni kuchanganya Kiwahili na Kiingereza kila unapoongea.
Mwisho nilikuwa nafikiri Kaka fredi, najua umefanya mengi duniani na hapa Tanzania angalia jinsi unavyoweza kutufikia na kutusaidia vijana wa uswazi hasa afya ya mwili upande wa mazoezi. Hii itapunguza utitiri wa vijana kufikiri kuwa kupata stimu lazima uvute bangi au madawa ya kulevya.
Asante
Renatus Mgusii