
Chuo Kikuu cha “St Augustine of Tanzania”
Leo nimepokea barua toka kwa mtaalamu wa jamii, habari, lugha na mpenzi wa nchi yetu, mwanae mhadhiri na msomi maarufu aliyefariki mwaka 2006, Profesa Chachage S. Chachage.

Prof Chachage, picha ihsani ya Blog la Isae
Kama marehemu baba yake, kila ninaposoma au kupokea maandishi yake, Chambi Chachage,… hufarijika. Mbali na mada muhimu anayoiongelea napenda alivyotafsiri maneno “magumu” ya kitaaluma toka Kiingereza kuja Kiswahili fasaha. Jambo hili ni muhimu ukizingatia Wabongo wengi (na Wakenya pia) tunaosema eti maneno ya Kiingereza hayana tafsiri ya Kiswahili. Tunatukuza Uswanglish badala ya lugha fasaha. Ebo! Hebu msomeni:
Ndugu Mwanazuoni Unayehusika Na Mada Hii,
Salaam za Saba Saba!
Katika ngazi ya Shahada ya Uzamivu (PhD) hasa kwenye Sayansi za Jamii (Social Sciences and Humanities) kilicho muhimu zaidi ni utafiti (research) ambao mwanafunzi ataufanya na tasnifu (thesis/dissertation) atakayoiandika. Hivyo sio lazima (sana) mtu awe kwenye fani fulani hasa kama hana mpango wa kuwa mkufunzi/profesa wa fani hiyo. Kwa mfano, ukifanya PhD hapa huwa unaruhusiwa kuchukua kozi kutoka kwenye idara/shule mbalimbali ili mradi tu uwe umechukua kozi za kutosha kutoka kwenye idara yako iliyohusika katika udahili (admission) wako chuoni. Hivyo, mimi mathalan nitachukua kozi za afya kutoka kwenye Shule ya Afya ya Jamii (School of Public Health), utawala kutoka kwenye Shule ya Tawala (School of Government), Sayansi ya Siasa, Fasihi, Stadi za Utamaduni na Jinsia, Historia, Saikolojia, Sosholojia, Anthropolojia n.k.

ila nikiwa nimelenga katika kufanya utafiti unaohusu masuala ya Afrika (African Studies) ambayo ndiyo fani yangu kuu niliyoifanyia shahada ya uzamili. Mpango wangu (ambao natumai hautabadilika kutokana na kuvutiwa na masuala/mada nyingi na hivyo kukosa mwelekeo(focus)) ni kufanya utafiti kuhusu namna ‘wasifu’ (identity) kama vile wa kimbari/kikabila/kiraia, kisiasa, kitabaka na kidini kwenye jamii unavyojengeka, unavyojikita na unavyobadilika katika – na kwa kutegemeana/kuendana na – muktadha wa migogoro anuwai juu ya rasilimali (natural resources).
Hapa PhD inasomwa kwa kufanya kozi kwa muda kisha ndio unaandika tasnia, ni tofauti na Uingereza na Tanzania (japo nilisikia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilikuwa katika mchakatao wa kuanzisha utaratibu kama wa Marekani ambao tayari Profesa Mamdani ameuanzisha kwenye Taasisi ya Tafiti za Kijamii Katika Chuo Kikuu cha Makerere (MISR)). Katika suala zima la kutuma maombi ya kupata udahili na skolashipu kilicho muhimu zaidi ni kulenga programu ya PhD yenye masuala yanayokugusa zaidi i.e. unayopenda na unayoweza kuyasemea. Natumai maelezo haya yatakusaidia katika harakati zako za kutafuta elimu na shahada pia.
Alamsiki,
Chambi wa Changanyikeni


Hii ni nzuri sana maana inatupa msaada sana hasa tulioko masomoni na hata walio kazini.
Nashukuru