
Juisi la Mbuyu ndani ya kitabu cha Miriam Rose Kitunda.
Miriam Rose Kitunda (pichani chini) ni mpenzi mkubwa wa utamaduni wa Kitanzania. Na mapenzi yake hayaishii tu kwa maneno na bla bla.
Kwa miaka mingi amekuwa akiwasaidia Watanzania kughani na kuziremba tovuti na blogu zao bila malipo yoyote. Hii ni kwa sababu kasomea ufundi huu wa kisasa. Halafu amekuwa akitangaza mapishi ya Kitanzania ndani ya tovuti yake www.tasteoftanzania.com Mwaka huu anatazamiwa kutoa kitabu cha mapishi hayo ndani ya kitabu moto moto cha Kiingereza na Kiswahili.

Ukweli hadi sasa tunavyo vitabu viwili tu vilivyoandikwa na Watanzania kuhusu mapishi ya Kibongo. Cha kwanza kilitolewa na Eva Pendaeli Sarakikya (TPH, Dar es Salaam, 1977) na Zarina Jafrejji katoa mapishi ya Zanzibar ( Taste of Zanzibar, Gallery Publications, 2006). Vitabu ni hivi viwili tu vinavyofahamika, vilivyoandikwa na Watanzania. Kwa hiyo ni furaha kubwa kujua kiko kingine jikoni na mekoni.
