Feeds:
Posts
Comments

Posts Tagged ‘LIlian Nabora’


Bongo ya joto, Bongo yenye kiu cha kujifunza na kujiendeleza.
Vijana walioparamia warsha chache nlizofanya Fasdo, Tandika, Dar es Salaam, Oktoba 2011 walikuja na maswali kem kem.
Walikuwepo washairi chipukizi wenye moyo na kujituma mathalan mwandishi Konisaga aliyesafiri toka Shinyanga kujua ataiendelezaje fani yake.

Kati ya Watanzania waliodamka na kuazimia kujijenga ni Mshairi Konisaga toka Shinyanga.

Walikuwepo watengeza sinema wabichi waliokuja kuduhushi wakitaka kuiendeleza fani hii inayoanza kuwaka na kukua Bongo.

Taswira za arsha hii ya siku mbili zilikamatwa na mpiga picha kijana anayejituma, anayehangaika, anayejitaidi, kujiendeleza, Tikyomo Stephen Chande (chini, kushoto) akinikabidhi kinywaji kitukufu yaani Madafu

Wacheza mpira pia waliwaka na kujitupa, kama yule aliyesumbuliwa na tatizo la musuli.
Au mzee mwenzangu, mtu wa makamo aliyesaidiana nami kuwatitimua vijana mazoezini siku jua lilipokuwa likiwaka utadhani tunachemshwa.
Wanawake walikuwa wachache lakini waliohudhuria walikuwa na maswali MAZITO.

Walikuwepo Watanzania wa kila namna, kabila na jinsia…na suala la unyanyasaji wa Ma Albino pia liliongelewa.

Swali mlima, swali simba, swali ugali, swali kuu la hizi warsha zote lilihusu maisha ya Ughaibuni.
Lakini sidhani Watanzania wanataka kuishi Ughaibuni. Wanachotafuta ni maisha bora. Ughaibu ina maana Uzunguni. Mazingira yanayosemekana yana ahueni, pesa, elimu, taaluma. Neno Majuu ni kigezo tu, chamb, ndoana.
Vijana wakiulizia je kazi zinapatikana Ughaibuni?
Je wafadhili wapo?

Gumzo kuhusu ufundi mitambo na matumizi ya zana za sauti na muziki…
Na hata siku mvua iliponyesha Tandika bado wapo waliodamkia, waliopambana na Dala Dala, miguu au hata teksi kuchimba, kufukua, kuulizia, kudadisi na kunusa harufu.
Ukweli kuishi Majuu hakuna maana majawabu KAMILI.


Nchi yetu ina kila riziki. Ndizi kisukari si tu ngumu kupatikana Majuu; aghali ajabu…

Maelezo kuhusu umuhimu wa mazoezi…
nchi yetu tajiri, nchi yetu imejaza kila aina ya rasilmali. Kinachohitajika ni watu wetu kuzidi kujipenda; na wale wenye taaluma nje na ndani kusaidiana kuichanusha Bongo yetu tamu na chungu kama asali na ndulele.

Mazoezi ya tamthiliya na uso…
Utajipendaje kama hujifahamu?
Kwanza kijue ulicho nacho: Kiswahili na ngoma zetu za Sindimba na Bugogobo. Tuuafiki uzuri wa mazingira yetu; kupitia milima Meru, Njombe, Usambara, Pare, Uluguru, Nguru, Kilimanjaro, Oldonyo Sambo…tuzitambue nyika, nyasi, miti, maziwa na mito, Rufiji, Wami, Mbu, Pangani, Victoria, Tanganyika; bahari ya Hindi, visiwa vya Mafia, Pemba; nyika zenye wanyama pori wanaovutia kila aina ya watalii…

Tanzania yenye riziki…tamaduni na Kiswahili…
Je tufanyeje kukidumisha na kukiendeleza Kiswahili chetu?
Je, Kiswahili kina faida gani?
Vipi wenzetu Waingereza wameifanya lugha yao kuwa dhahabu, wanja na manukato ya ajira yao? Kwanza wametambua uzito na thamani ya lugha hii. Wanaendelea kuwatukuza waandishi wao, akina William Shakespeare na mwanariwaya Charles Dickens. Waingereza wanaitukuza lugha yao kiasi ambacho wamekuwa wavivu (ingawa si wote) kujifunza lugha za wenzao. Sisi wengine (na wenzao) ndo tunaopigania kujifunza kimombo. Hadi kujidunisha wenyewe…


Watalii katika boti la Zanzibar wakijitahidi kupiga picha. Nchi yetu inapendwa kwel kweli.
Picha na mdau wa Kitoto…
Kwanini sisi wenyewe tukubali idunishwe?
Kiswahili chetu si lugha ya kabila moja. Kiswahili chetu kinaweza kuwa ajira, kinaweza kuwa hazina, kinaweza kuwa ufunuo wa njia zilizozibwa.
Watanzania lazima tusome riwaya na fasihi zetu tuandike na tutukuze wasanii wanaokiimba Kiswahili kwa Bongo Fleva, Taarabu au hata nyimbo za dini.
Hilo lilikuwa moja ya gumzo kuu la semina hizi.
Kulizungumziwa pia suala la kufahamu taaluma ya elimu viwanda, sayansi na teknolojia. Vijana wa Fasdo waliulizia namna ya kuendesha mitambo ya kuendeshea muziki, sinema na maonyesho ya jukwaa.

Ujuzi dhoofu na finyu wa mitambo ni sayansi inayozifanya kazi zetu Waafrika kutoonekana maridadi. Kumbe safi kabisa na zina uwezo na hatima ya kupendeza na kutukuka ndani ya sayari yetu

… sisi Waafrika wazuri wa sura, wazuri wa mandhari, tumeiva kwa visa na maisha kama walivyowenzetu wengine ulimwenguni.
Kutokana na taaluma dhaifu iliyoko katika picha na taswira zinazoonyeshwa katika sinema, muziki na kazi nyingine tunaonekana dhaifu.
Kumbe sivyo.

Sayansi hii iliongelewa pia.
Nawashukuru Chande Nabora, mwanae, Tikyomo, dadake Lilian Nabora na mkewe Chande aliyetupikia misosi siku hizo mbili…

Read Full Post »

Mdau wa Kitoto natazamia kufanya semina mbalimbali za afya, mazoezi ya viungo, muziki, fasihi, lugha nk katika ukumbi wa Fasdo ulioko Tandika, Dar es Salaam; Jumanne tarehe 11 na Jumatano tarehe 12 Oktoba, 2011.Wote mnakaribishwa…


Moja ya shughuli lukuki zinazofanywa na kituo hiki cha maendeleo ya sanaa na michezo ni utengenezaji wa vitambaa vya Batik, vilivyofanywa na akina mama wa Fasdo.
Picha na Lilian Nabora

Kiingilio bure.
Habari zaidi wasiliana na Chande Nabora, Mkurugenzi wa Fasdo. Simu namba 0713-310-755 au Nasibb 0713-261011.

Darasa la utengenezaji wa sabuni….
Picha na Lilian Nabora na Ticky Tedvan.

Tembelea tovuti yao : http://www.fasdotz.com


Darasa la kuimba.
Picha na Lilian Nabora


Mfano wa warsha za mazoezi na afya ya mwili mdau niliyofanya Nyumba ya Sanaa mwaka 2009.
Picha na Innocent Swai.

Read Full Post »