Feeds:
Posts
Comments

Posts Tagged ‘Mazingira’

Saa tisa na nusu alfajiri. Nimetoka nje kuangalia hali ikoje.
Njia iliyonyeshewa London
Watabiri wa hali ya hewa wamesema leo asubuhi ya kuamkia Jumatatu, Uingereza “itakiona cha mtema kuni.” Upepo mkali wa bahari ya Atlantic utapita zake na kimbunga, tufani na dhoruba. Wameonya wananchi kutotoka toka labda tuwe na lazima. Kawaida saa hizi huwepo magari na watu wakipita pita barabarani, mtaa nnaoishi.
Karibu ya hapa mna mabaa na vijitoheli hoteli vya Waturuki (nyama choma “donner-kebab”- za kondoo). Lakini sikuona mguu, jicho, wala kiatu. Nadhani kila mtu kanywea zake kitandani, akisikiliza upepo na matone ya mvua madirishani…

Read Full Post »

Wamesema mara ya mwisho baridi kali namna hii kutokea visiwa vya Uingereza ilikuwa miaka 30 iliyopita.
Leo kila mtu nliyekutana naye jijini: mzee, mtoto, mwanaume, mwanamke, alilalama na kulaani baridi.
Baridi imedoda-2
Hata “maglovu” nliyovaa mkononi hayasaidii. Ngumi haikunjiki sawasawa. Mti kule nyuma umepukutika matawi- zimebaki tu kuni kavu. Ndevu zangu zimenyang’arika. Upepo wa kutoboa kisindano sindano ulikuwa ukisaidia baridi kuwa nyuki zaidi.

Aliyewazidi wote kwa malalamishi alikua ajuza mmoja mzawa wa visiwa vya Karibian. Alihamia hapa miaka 55 iliyopita.
“Nlikuja kusoma na kutafuta ajira. Sipendi na siizoei baridi hata kidogo.”
Nkamuuliza kama haipendi baridi kwanini harudi tu kwao kwenye ujoto joto?
Basi la London
Basi linapitisha abiria waliojikunyata ndani.

Ajuza akajibu keshapazoea; lakini asichokiweza baridi.
Rudi basi kwenu.
Ajuza akacheka.
(more…)

Read Full Post »

Leswin Rd-with snow
Miti na magari yametota barafu utadhani maziwa mgando.

Si kawaida sana kuona barafu London- lakini kwa mara ya pili mwaka huu barafu hilo limeshuka tena.
Kawaida barafu inapoanguka baridi kiasi fulani hupungua.
Tatizo ni wakati ikianza kupungua kunakua na utelezi; watu wengi hasa wazee na akina mama hudondoka dondoka na kuvunjika mikono na miguu.
London Buses
Mabasi ya ghorofa London

Lakini maisha lazima yaendelee. Wanasema eti ilibidi Wazungu waendelee haraka shauri katika hali kama hii huwezi ukalala; ukizubaa unashindwa na maisha. Ndiyo maana wakawa wachapakazi.
Mfagizi anaondoa barafu njiani
Mfagizi wa barabara akikwangua barafu ili kurahisisha watu kupita. Katika nchi zilizoendelea ukianguka unaweza kudai halmashauri ya mitaa au jiji malipo ya bima. Hii ni kwa sababu kodi unayolipa inatakiwa ilipie mazingira yanayokuzunguka kwa huduma kama za huyu bwana hapa.

(more…)

Read Full Post »

Moja ya jambo kubwa sana ulimwengu wa sasa ni kuyajali na kuyahifadhi mazingira. Ukiutazama mji wa Dar es Salaam ulivyoharibika leo kutokana na 1. Msongamano wa magari 2. Mioshi na vumbi inayotakana na magari, mashine na barabara mbaya 4. Kutupa taka ovyo (hasa mifuko ya plastiki na chupa) kila mahali 4. Mpangilio mbaya wa ujenzi wa nyumba…
Utagundua kuwa mji umeshapoteza wajihi wake wa zamani. Jina asilia la Dar es Salaam lina maana “Bandari ya Salama” ; je usalama bado upo? Na je kama unafifia tutauokoa vipi?

Mwana Kitoto nikiwa eneo la Tangi Bovu mwaka 2009; hapa karibu walikuwa watoto wakicheza, maduka na makazi …kila mtu pale mstaarabu, muungwana lakini mazingira yakiumia. Picha na Innocent Swai.
(more…)

Read Full Post »

Mei 2009 niliendesha warsha kadhaa Dar es Salaam, zilizoongelea mada mbalimbali; mosi ilikuwa hii pale British Council.

SEMINA 1- Ughaibuni

“HAITOSHI WEWE KULIELEWA, BALI NA WEWE KULIELEZEA NA MTU MWINGINE AKAELEWA…”
-Profesa Chachage S. L. Chachage, “Makuadi wa Soko Huria” , 2002.


Usafiri usiotegemea magari unazidi kutakiwa Majuu; upandaji baiskeli unapewa kipaumbele kwa kuwa hauchafui mazingira kwa uchafu wa moshi na petroli. Picha ya mtaa wa Tottenham Court Road, mjini London na F. Macha

Vijana na baadhi ya wazalendo leo wanataka kwenda nje kusoma, kufanya kazi au kutembea. Kinachotusukuma kwenda nje ni mseto wa uchumi mbaya, umaskini na kutaka tu kufahamu mambo. Lakini je, hili ni jambo geni? Kutaka kwenda Ulaya, Marekani, Afrika Kusini au Australia hakukuanza leo.

Ari ya kuhama hama ni moja ya nguzo kuu za uhai wetu wanadamu.

• KUHAMIA UGENINI NI JAMBO LA KAWAIDA

1-Migogoro na Tafrani husababisha kuhama:
Hakuna kipindi katika historia ya maisha ya wanadamu ambapo wananchi wowote katika nchi yeyote ile duniani hawakuhama ama kwa sababu za kivita, migongano ya mali (ardhi, biashara, nk) au kutafuta tu kazi na maisha bora.
Umri wa ulimwengu ni miaka 6,000. Katika kipindi hicho vita mbalimbali zimefanywa na kusababisha watu kuhama. Asilimia 70 ya vita zimetokana na sababu za Kidini, Mbari na Ukabila (1). (more…)

Read Full Post »


Mholanzi, Willem Nolens, akisifia namna Tanzania ilivyo mstari wa mbele katika medani ya umeme huu unaotumia jua na ambao utaondoa nuksi ya “mgao wa umeme” ,  dhiki ya tanesco na kurahisisha maisha ya wengi, hasa vijijini.  Mwangalieni Baraka Baraka wa “Urban Pulse” akiwa kazini na kamera yake.

(Picha na F Macha)

Serikali za Afrika Mashariki zimeombwa kuendelea kuunga mkono jitihada za kujenga umeme unaotegemea jua na mali asili kwa kuwa ni wa bei nafuu na rahisi zaidi kutumiwa na mamilioni ya wananchi vijijini.

Wakiongea nami mwanzoni mwa juma hili, washindi wa tuzo linalotolewa kwa wanasayansi waliobuni mbinu za kusaidia mazingira na thamani ya maisha ya jumuiya , mjini London, walisisitiza haja ya serikali zetu kuamka maana mitambo hii ni suluhisho la tatizo kubwa la umeme.

Tuzo la Ashden hapa Uingereza,  hutolewa kila mwaka kwa wananchi wanaosaidia vita vya kuleta mabadiliko ya mazingira. Tuzo hiyo iliyoanzishwa mwaka 2001 na Bi. Sarah Butler-Sloss wa duka  la tajiri mashuhuri wa Kiingereza, Lord Sainbury humzawadiya mshindi wa kwanza paundi 30,000 na wawili wengine 20,000 kila mmoja.

Mwaka huu washindi husika wametoka Kenya, Uganda, Marekani, India, Vietnam, Brazil na Uholanzi.

Msemaji wa Ashden, Mariana Mazonen, mzawa wa Mexico alisema kila mshindi husika kasaidia kubuni njia za kutengeneza umeme kwa njia zinazopunguza mategemeo ya mkaa, miti na mafuta ya taa au petroli.

Akiongea nasi, mshindi toka Kenya, Samwel Kinoti, wa kampuni ya Sky Link, alieleza kuwa nchini wamekuwa wakiendeleza matumizi ya kinyesi cha ng’ombe kutengeneza umeme.

Mtaalamu,  Samwel Minoti akifafanua namna sayansi ya kutumia kinyesi cha ng’ombe kutengezea umeme na mwangaza unavyoanza kuwafaidia wananchi wa Kenya (Picha na F Macha).

Kenya ina upungufu wa matumizi ya miti ambao ni asilimia 1.59 tu. Hii ni chini ya asilimia kumi inayotakiwa na Umoja wa Mataifa. “ Wananchi wengi wa Kenya bado wanaegemea miti na mkaa ambavyo ni aghali sana. Sky Link inajaribu kurekebisha tatizo hilo kwa kueneza matumizi ya gesi ya Biogas kwa shughuli za upishi,” alifafanua Kinoti toka Meru.

Akionyesha namna taa za umeme wa jua zinavyokuwa mtengezaji wa D Light inayopata nguvu toka jua, Ned Tozun toka Marekani alisema yeye na mwenzake Sam Goldman waliunda vifaa hivyo mwaka 2007.

“Uvumbuzi umekua haraka kiasi ambacho sasa hivi tunazo ofisi Hongkong, India, Tanzania na Marekani.”

D Light inasisitiza kuwa leo duniani wapo watu bilioni moja na nusu wasiokuwa na umeme.

“Wengi bado hutegemea mafuta ya taa. Mwangaza huu ni aghali, unaharibu mazingira na si mzuri kwa afya. Familia nyingi zinapata shida kuafikiana na gharama hizi. Matumizi ya mwangaza unaotegemea jua ni rahisi kwa nchi kama Tanzania ambazo zinazokuwa na jua kila wakati.”

Akionyesha  vifaa alivyounda na mwenzake, Bwana Touzen alisema si aghali na ni rahisi kutumia. Kiran mathalan inafanana na tochi lakini ina mwangaza unaotosha kumulika chumba kizima kama taa za kawaida  tulizozizoea za umeme.

Mtaalamu wa Kimarekani, Ned Tozun, akimfafanulia Baraka Baraka  namna umeme huu wa jua na mali asili unavyotumika kirahisi, mjini London, Jumatatu.  Tanzania ni moja ya nchi chache duniani zenye ofisi ya kampuni ya D Light.

(Picha na F. Macha)

Washindi wengine wa tuzo la Ashden ni Chris Mulindwa toka Uganda na William Nolens wa Uholanzi. Hawa wanawakilisha shirika la Mwangaza Vijijini (Rural Energy Foundation) ambalo limeshajenga kazi zake Tanzania pia.

Wanasisitiza kwamba asilimia 95 ya vijiji vya Afrika vinahitaji huduma hii.

“Bila umeme, si rahisi wananchi kuendelea. Wananchi wanatumia pesa nyingi kununua betri na mafuta ya taa. Wanashindwa kuona runinga na mawasiliano mengine kama simu. Uhaba huu unazuia maendeleo yao.”

Chris Mulindwa( kulia) Mganda anayefundisha masuala ya biashara na sayansi hii, akiwa na mdau wa Kitoto.

(Picha na Baraka Baraka wa Urban Pulse)

Read Full Post »

Si mara nyingi mji wa London kuangukiwa na barafu kama sehemu nyingine za Ulaya…ila inapodondoka kila kitu husimama. Mpiga picha wetu maarufu, Kiondo W. Kiondo, lakini hakusimama. Leo alfajiri, kajikongoja hadi uwanja wa ndege maarufu wa Gatwick (mbali kwel kweli) katuletea taswira hii.  Ole wenu mnaotaka kuja Ughaibuni, mkidhani humu zimo almasi, asali na mbingu tupu. Hii baridi si ya mchezo. Inauma.

Tuache utani…

Wanasayansi na wataalamu wa tabia hupenda kusema Mzungu eti  “alituzidi akili” au kuendelea kutokana na mapambano yake na mazingira zamani. Katika hii baridi ukifunga macho, ukisimama dede, ukijikunyata, usipofyatuka na kuharakisha kimwili na kiakili unakufa…

Read Full Post »

Older Posts »