Juma hili habari kwamba kitabu kipya cha mwandishi nguli, Adam Shafi (Kasr ya Mwinyi Fuad,Kuli, Vuta Nkuvute na Haini) kimetoka ni za kushangilia sana. “Mbali na Nyumbani” inaangalia maisha yake msanii huyu Ughaibuni takribani miaka 50 iliyopita…Kimetolewa na Longhorn Publishers wenye makao yao Nairobi Kenya na matawi mbalimbali Dar es Salaam, Kampala na Rwanda.
Mara ya mwisho nilipomhoji Mzee Shafi, Desemba 2007 alikuwa bado anakiandika kitabu hicho ambacho alisema kitaelezea maisha yake ya ujanani.
Shafi akiwa na mjukuu wake Lowell, mjini Milton Keynes, Uingereza. Picha na F Macha
Katika uchambuzi wa kitabu hicho, mwandishi hodari wa Kenya, Profesa Ken Walibora, anasema mtindo wake wa kuangalia tawasifu- ambapo mwandishi au mhusika anaelezea maisha yake haujaenea sana katika maandishi ya Kiswahili seuze ya Kiafrika. HIvyo anasema Walibora, ni jambo zuri la sisi wengine pia kulifanya.
Mbali na kutukuza kitabu hiki, Profesa Walibora anachangamkia namna maandishi na lugha ya Kiswahili inavyoendelea kukua duniani. Hivyo kututaka Waswahili kuendelea kuandika na kujenga na kuimarisha KISWAHILI.
Mwanafasihi Shafi akinionyesha muswaada wa kitabu hicho -wakati kikiwa bado jikoni miaka mitano iliyopita.
Ni jambo la kuchangamkia kwamba kimemalizika. Picha na F Macha.
Kuli, kilichotolewa mwaka 1979 (TPH) na 2005 na Longhorn, ni moja ya vitabu maarufu vya mwandishi ambavyo vimempatia sifa ya kuiangalia jamii yake kwa macho ya darubini kali ya kimaendeleo.
Kasr ya Mwinyi Fuad, toleo lake la kwanza kabisa, lilitolewa pia na TPH mwaka 1978. Kitabu hiki kimeshatafsiriwa katika Kifaransa, jambo linaloonyesha namna mwandishi huyu anavyosifika duniani.
SOMA TAHAKIKI YA PROFESA KEN WALIBORA (aliyehariri na kuchangia kitabu kizuri sana cha Kiswahili, pamoja na Profesa Said Ahmed Mohammed, DAMU NYEUSI, kilichotolewa na MacMillan Kenya, 2007!)
http://www.swahilihub.com/habari/MAKALA/-/1310220/1672466/-/ouhmen/-/index.html