Ijumaa tarehe 30 Mei, London.
Ukumbi wa hoteli iliyoko kitongoji cha Hackney, kaskazini ya London ulishuhudia usiku wa muziki, chakula na vinywaji.
Kila aliyeingia hapa alifahamu alichokijia. Hakukuwa na hotuba wala kelele nyingi. Mabango yaliyopitishwa miezi kadhaa yaliibeba bendera ya Tanzania na wito wa “NYIMBO KWA DADA ZETU”…matangazo yalienezwa sehemu mbalimbali London na mtandaoni. Wapenzi wa Tanzania weupe kwa weusi waliitikia wito.
Majina ya wanamuziki pia yalitangazwa na mgeni rasmi wa shughuli hii alikuwa dada Malkia Kassu, mshindiw a taji la Miss Commonwealth Afrika 2013. Bi Kassu alikuwa na wadhifa wa kusimama mbele ya meza iliyotangaza habari mbalimbali za Tanzania akiwa kavalia taji lake na kusaidia kutangaza mshindi wa bahati nasibu (raffle) ya usiku huu.
Malkia Kassu akionyesha taji lake linaloitangaza Afrika na Tanzania. Picha na See Li.
Shughuli ilifana.
Baadhi ya wahudhuriaji wa shughuli. Picha ya See Li.
The Russet lilijazana wanawake kwa wingi (wa mataifa mbalimbali), wanaume pia walikuwepo.
Ukeketaji wa wanawake ni adha inayoendelea kupingwa na kupigiwa kelele ulimwengu mzima.
Wahudhuriaji wa tafrija la The Russet. Picha na See Li.
Nchi husika ni Afrika, Mashariki ya kati na Asia. Ukeketaji pia unaendeshwa na wageni waliohamia nchi za Uzunguni, hususa, Marekani, Canada, Ufaransa, Uingereza nk. Kufuatana na takwimu za shirila la Afya duniani (WHO) wanawake milioni 91 na nusu barani Afrika wamekeketwa. Kati ya hawa milioni 12 na robo wana umri mdogo wa miaka 10 hadi 14.
Nadia Al Faghih Hassan, mpiga ngoma toka Libya akitumbuiza. Picha ya See Li.
Tovuti la FGM linadai nchi 26 za Kiafrika ikiwemo Tanzania zinatekeleza adha hii kwa kina. Watetezi wake ni wanawake waliokeketwa na baadhi ya wanaume. Adha kwanini? Madaktari Tanzania wameonya asili mia 50 ya wasichana wetu yamo hatarini. Hatari zipi?
-Kuvuja damu ovyo maisha yao yote
-Maumivu nyakati za haja ndogo na kubwa
-Maumivu siku za hedhi na uja uzito
– Hatari wakati wa kujifungua
-Kutozaa. Uchunguzi uliofanywa Sudan (moja ya nchi ongozi za desturi hii muflis), umethibitisha utasa na kutozaa kwa asilimia ya wanawake 25.
-hatari ya kufa kutokana na majeraha haya
Mwanamuziki Lora Linhares Max akitumbuiza. Picha na See Li.
Watayarisha wa shughuli ya The Russet walikuwa Janet Chapman na Jonathan Pace, toka Tanzania Trust Development Fund ambao ni mkono wa shirika la Urafiki baina ya Uingereza na Tanzania (British Tanzania Society).
Janet Chapman.
Janet na Jonathan wamedhamiria kutafuta paundi 60,000 (takriban shilingi 200,000). Fedha hizi ni za ujenzi wa jumba la kuwasaidia na kuwakomboa wasichana wanaokimbia ukeketaji, Bugumu, mkoani Mara, Tanzania.
Jonathan Pace.
Ingawa jumba linaendeshwa na kanisa la Angilakana, watu wa madhehebu yote watakaribishwa.
Pale wasichana watafundishwa:
– useremala
-kushona
-kutumia tarakilishi (kompyuta)
na elimu nyingine za kuwasaidia maisha yao ya baadaye.
Julian Marcus wa British Tanzania Society, akionyesha shati la Kiafrika. Alikuwa na meza iliyojaa habari mbalimbali za Tanzania. Picha ya See Li.
Tafrija hii ya Mei 30 – ilimudu kupata paundi zaidi ya 1,000. Watayarishaji wameweka vitabu vyao wazi na kusema sherehe nyingine itafanywa Oktoba, baadaye mwakani, kuendeleza michango. Tutakiane kheri.
Sokoshumba – wanamuziki toka Zimbabwe wakiimba nyimbo za jadi kwa marimba na sauti nyororo zilizopangwa vyema.
Picha ya See Li.
Janet na Jonathan walisema walifurahishwa na mahudhurio makubwa yaliyoonyesha kuunga mkono harakati dhidi ya ukeketaji.
Mdau wa Kitoto nikitandika ngoma, siku hiyo. Picha na See Li.
Leave a comment