Nimepokea simu. Simu ya maana. Adam Shafi yuko Majuu. Kaja kikazi Uholanzi. Yeye mtaalamu wa lugha ya Kiswahili. Baada ya kumaliza kapitia Uingereza katika mji mmoja wenye wakazi wengi wa Kitanzania, yaani Milton Keynes. Ni wastani wa saa moja kwa treni toka London. Mrefu, mchangamfu, mzungumzaji aliyesheheni “mastore” kibao. Nishakutana na waandishi wa kila sampuli. Wanaojificha: wakimya, wasioongea sana, wapole wanaokaa chumbani kati kati ya watu ukadhani hawapo. Wanaopiga kelele, wakijafaragua; ama wenye aibu…
Shafi ni mtu wa kawaida kabisa, naweza kuiita hulka, tabia na namna yake “Mfurahia Maisha” : kachangamkia uhai, haswa. Kaishi, anaishi…hamalizi. Kila mara atasema ana mikakati ya kufanya jambo fulani, kuandika kitabu kingine kipya, kuendeleza fasihi na Kiswahili….
Katika saa nne zote nlizokuwa naye ananikumbusha moja. Ikiwa umewahi kuvisoma vitabu vyake utagundua huchanganya kila kitu: furaha, simanzi, vita, amani, mapenzi, karaha, starehe, maonyo, mandhari, elimu na mengine tele. Ukiongea naye yuko hivyo hivyo. Mastore kibao. Anaelezea namna wachapishaji waliotafsiri moja ya vitabu vyake walivyotaka kumrusha fedha. Akawafungia safari hadi Paris kudai haki hiyo. Au alivyofiwa na mpenzi wake wa ujanani zamaaaani…pamoja na mtoto. Alivyotiwa jela ugenini ujanani (anamalizia kitabu kipya kuhusu kisa hiki, soma mbeleni); alivyofungwa Unguja baada ya mauaji ya Rais Karume. Hadi leo mguu wake wa kushoto ananionyesha bado una dosari (“pana ganzi pajani shauri ya kulala sakafuni”); alifungwa miaka miwili. Visa, kibao. Vyote vimepenyezwa angalau kiduchu ndani ya vitabu vyake. Vingine vishatafsiriwa lugha za kigeni. Kimoja kilishinda tuzo. Niko naye. Tunakula ubwabwa uliopikwa vizuri na binti yake kwa nyama za kukaanga…huku tukila huku tukiongea. Mazungumzo hayaishi. Ingawa masaa manne mengi kukaa na mtu (kwa huku Ulaya ambapo muda ni dhahabu) nahisi itabidi nipewe miezi ili kujua mengi zaidi ambayo nataka kuyafahamu. Anachonifurahisha ni hii picha akiwa na mjukuu wake wa miaka minne. Huyu ni mtu aliyeshaishi. Akaona mengi. Akazaa. Akalea. Aka…mcheki.
Waandishi ni watazamaji na wasikilizaji wakubwa wa jamii. Waandishi ndiyo hutukumbusha yaliyotokea. Kusingekuwepo waandishi tusingefahamu yaliyopita. Kila mmoja wetu kila siku anahangaika na maisha. Tunaamka, tunakula, tunakwenda kazini au masomoni. Tunarudi , tunalala, kesho yake hayo hayo: kila kukicha na kuchwa tunaona mengi, tunayapita, tunayasahau. Ila waandishi? Wasanii? Kazi yao kuweka kumbukumbu ya haya mambo. Kuyahadithia. Wapo waandishi wa aina nyingi. Wana habari. Waandishi wa elimu na historia. Washairi. Watunzi wa muziki na nyimbo. Sinema. Tamthiliya.Wapo waandishi wa fasihi kama Adam Shafi. Shafi alianza na kitabu cha “Kuli”, kinachoelezea mgomo maarufu wa wafanyakazi maskini , Unguja mwaka 1948. Anasema alikuwa na miaka minane tu. Na ingawa anakumbuka juu juu tukio hilo utotoni, alikuja kuhaditihiwa na mtu akaweka kumbukumbu na baadaye maandishini. (Unaona waandishi walivyo watu muhimu, kutukumbusha?)
“Kuli” kilichapishwa na Tanzania Publishing House (TPH) miaka ya Sabini. Lakini awali alichapisha “Kasr ya Mwinyi Fuad” ambacho kimeshatafsiriwa lugha tatu za kizungu: Kijerumani, Kifaransa na Kirusi.
Miaka ya karibuni, Shafi kaibuka na “Vuta Nkuvute” kilichopata Tuzo kwenye tamasha la vitabu, Dar es Salaam, mwaka 1998. Ni kisa cha mapenzi, tena mapenzi makali na mazito kati ya msichana wa Kihindi na Mwafrika. Humo mna siasa na harakati za uhuru na mengi mengine. Mseto mkubwa wa mapenzi na siasa, ambao si waandishi wengi wa KIswahili wamemudu kuuchanganya.
“Vuta Nkuvute” kilichapwa na Mkuki na Nyota. (Soma habari zao hapa : http://www.mkukinanyota.com) .
Mwaka 2003 mwanafasihi huyu alitoka na “Haini” ambacho kama anavyosema mwenyewe kiliogopwa na wachapishaji wengi nchini. “Haini” si mchezo. Kitabu cha moto, cha kuchachafya. Soma ukurasa wa kutisha wa mfungwa mmoja akipambana na chatu, ukurasa wa 172:
“Anaiangalia dunia kwa hofu na kukata tamaa, anachungulia kaburi. ..Alipomtazama yule chatu alimwona anaanza kujinyumbua, ananyeka, kichwa amekiinua,kama anayezindukana kutoka usingizini. Chakula chake amekwisha andaliwa, hana wasiwasi. Tayari kimo mle chumbani.”
Kama desturi visa vyote vya Shafi hujaa mateso, shida, majonzi, taabu za Mwafrika; lakini haviishii na hisia hizi za kukata tamaa na kutokwa machozi. Wahusika wake huteseka lakini mara wakaibuka, wakaamka na kupambana na matatizo yao. Matumaini ndiyo rangi ya suluhisho lake.
“…Moyo wa ujabali ukamjaa tele akahisi na nguvu kama za simba yuko tayari kuvaana na chatu yule kwa mikono yake miwili. Chatu naye amenyanyua kichwa anajiramba midomo. Huutoa ulimi wake halafu akaurudisha ndani na pale anapoutoa utadhani anatoa miali ya moto kutoka mdomoni. Wanatazamana. “Nani atakayeanza kushambulia?” Haramia anajuliza.”
Msomaji sin’takueleza yaliishia wapi. Maana ukijua hutatamkiwa kitabuni. Nnachokumbuka sikulala baada ya kusoma sura hii. Inatisha. “Haini” ni kitabu kinachosisimua sana. Kilinikumbusha visa vya mwandishi wa Kimarekani Stephen King, ambaye karibu vitabu vyake vyote vishafanywa sinema. Sinema yake maarufu ni ile ya kutisha sana iitwayo The Shining. Sidhani ntakosea nikisema maandishi ya Shafi hayapishani na waandishi wa aina hii hata kidogo. Vikitafsiriwa vitapendwa ulimwenguni kote. “Haini” yahusu namna Shafi alivyofungwa jela miaka miwili akiwa bado mwandishi wa habari (taaluma yake kikazi)…akifanya kazi gazeti la “Uhuru” ambalo enzi za miaka ya Sabini (alipowekwa kizuizini) visiwani liliitwa “The Nationalist.” Ubaya,walakini, mmoja. Kitabu hiki kimechapishwa Kenya na Longhorn (http://www.longhornpublishers.com). Bongo hakipatikani kirahisi bali duka moja tu mitaa ya Kinondoni.
Vitabu vyake vyote Shafi vinaonyesha maisha ya sasa na yale yaliyopita. Anapenda kuhusisha historia ya jamii. Kwa hivyo mbali na kustareheshwa unafahamishwa mambo yaliyopita ya zamani. Hali hiyo imo pia katika muswada wake mpya “Mbali na Nyumbani” ambao unaelekeza maisha ya ujanani wa mwandishi.
Namsikiliza mwanafasihi huyu aliyezaliwa Unguja mwaka 1940 akinisomea: “Mbali Na Nyumbani.” Anasema huchukua wastani wa miaka mitano kumaliza kitabu kimoja. “Huwa sina haraka hata kidogo…” Huandika kwanza kwa mkono halafu ndiyo akachapa katika tarakilishi (kompyuta)….”Mbali na Nyumbani” anafafanua, kinasimulia ujana wake kati ya mwaka 1960 na 1967 …akijaribu kuvuka Afrika kwenda Ulaya. Hapa alipo ukurasa wa 427 (cheki picha juu)anasimulia akiwa mpakani Sudan kuingia Misri. Anaposoma ananikumbusha mwaka 1978 nilipojaribu na mimi kustoawei kwa meli. Vijana enzi hizo tulitaka sana kupanda meli. Ubaharia ulikuwa kazi ya kutamanika, kutafutwa na kuotea. Miaka hiyo imepita. Leo Vijana bado wanaotea kuingia nchi zilizoendelea. Nchi za Magharibi. Maisha yalikuwa magumu enzi zile, bado magumu leo, miaka arobaini na sita baada ya Uhuru. Lakini Wazungu wamefunga mipaka. Hawataki wageni. Enzi hizo ilikuwa vile vile. Kupata “kitabu”ilikuwa kazi; leo pia iko kazi. Kupata visa ilikuwa kazi; leo pia iko kazi.
Miaka kumi na mitano iliyopita mtindo uliibuka kwa Mwafrika kujifanya mkimbizi. Hiyo ziku hizi imeshatafutiwa ufumbuzi. Wazungu washajua. Washajua mathalani kuwa Bongo hakuna vita. Yalipokuja mauaji na machafuko ya Burundi na Rwanda wengi tukaanza na sisi kujifanya wakimbizi kutoka sehemu hizo. Ujanja huo ulifaa hadi miaka michache iliyopita. Leo yamegeuka. Wahusika washagundua. Ukimbizi leo haufai tena kama sababu. Yuko jamaa kanieleza ujanja mpya. Kujifanya junya au firauni. Si mnajua tena kuwa jadi hii nchi za Kizungu inaruhusiwa? Mwanaume kuoa mwanaume au mwanamke kumwoa mwanamke mwenzako?
Mwezi jana ilipitishwa sheria Uingereza kuwa ukishtakiwa kuwa umemtania msenge au firauni unakwenda jela miaka Saba. Vituo mbalimbali vya polisi vina vitengo maalum vya kutetea maslahi ya wasenge, na vinaongozwa pia na polisi wasenge. Basi kusikia hayo walala hoi nao wamegundua mpya. Afrika tabia hii hairuhusiwi wala si mila yetu. Basi ukitoka kwenu ukisema umeteswa kwa kuwa wewe msenge, ah unakaribishwa mikono miwili. “Kwani watakucheki?” anauliza mpambe aliyenieleza. “Watakucheki vipi? Watakufungua makalio?”
Basi, ndoto na njozi za kutoka Afrika kwenda Majuu hazikuanza leo. Kitabu kipya cha Mzanzibari Shafi, kitaonyesha harakati hizo miaka ya zamani kabla wengi hatukuzaliwa. “Mbali na Nyumbani” anasema kimeshauliziwa na wachapishaji kadhaa hapa Bongo na Kenya. Pichani chini Adam Shafi akinisomea muswaada.
Lakini swali niulize. Wangapi wanamfahamu Adam Shafi? Kwa wasomaji wa vitabu vya hadithi na fasihi, jina hili ni la kusisimua na kuvutia. Kwa wapenzi wa lugha yetu tukufu ya Kiswahili huyu ni mjumbe. Walii. Tarishi. Al Watan. Mpiganiaji. Mbunge wa lugha hii. Ndugu msomaji nikupe mfano? Hebu kumbuka Wabongo wangapi wanaodai eti hawana msamiati wa kutosha kujielezea Kiswahili. Utamsikia mtu kasoma, ana shahada, ana ujuzi na utaalam wa hali ya juu akisema : “Ah siwezi kuandika barua kwa Kiswahili…” Ilhali (lakini) anaongea Kiswahili fasaha lakini kuandika anashindwa. Anatumia Kiingereza. Kiingereza chenyewe marea nyingi kibovu. Afadhali hicho Kiingereza kingekuwa kizuri. Msikilize babu na gwiji wa fasihi ya Kiswahili, Ustaadh Shaaban Robert akituasa katika Utenzi wa Adili:
“…Lugha humpa hadhi
Kutumia ajuaye.”
Kisa cha kusema haya yote nini?
Ukitaka kuboresha lugha, ( yeyote ile) soma vitabu. Soma hadithi. Soma mashairi. Kama vile ambavyo wanamuziki hujiendeleza kwa kusikiliza miziki ya aina mbalimbali, msamiati, lahaja na lugha huendelezwa kwa kusoma vitabu. Kwako msomaji unayegomba huwezi kujieleza vizuri kwa Kiswahili, au kuandika Kiswahili…katafute vitabu vyake Adam Shafi, utafaidika na kustareheka.
Watanzania tunasemwa hatusomi. Baa ziko nyingi kuliko maduka ya vitabu na maktaba. Taifa lenye watu wasiosoma linajichimbia kaburi la ujinga.
Nikiwa na Shafi, mjini Milton Keynes alipopitia juma lililopita. Picha imepigwa na Hawa Yaxley.
Hebu onja (kidogo) baadhi ya ubingwa wake wa matumizi ya lugha katika nukuu zifuatazo (hapa ni vitabu viwili tu):
“Alihisi Shihab alikuwa kama aliyemtupia mshipi akaumeza pamoja na ndoana, chambo na chubwi.” (Vuta Nkuvute).
“Aziz alitaka kuibusu midomo ya Khadija. Amemwinamia, uso umembadilika, uchu wa mwanamke umemtawala akili zake zimehama kutoka kichwa cha juu zimehamia kichwa cha chini. Alipotaka kumbusu Khadija alimtemea mate yakamtapakaa uso mzima. Alimwachia mkono mmoja ili ajipanguse yale mate, Khadija akaukamata mkono wake akaung’ata, Aziz akasikia maumivu makali yakipanda mpaka utosini.” (Haini).
“Midomo aliitafuna tafuna nakuimungunyua mungunyua kama mtafuna tambuu…” (Vuta Nkuvute).
“Tokea siku ile aliposokomekwa ndani mle, furaha kwake ilikuwa adimu na huzidi kugubikwa na majonzi pale anapowaza kwamba kosa alilolifanya ni kule kuchinja jogoo lake mwenyewe…” (Haini)
“Amle Mbiza, amle Mboza? Aliwaona kama wote wawili wamemsimamia mbele ya macho yake, achague mmoja. Huyu mmoja keshaolewa, mke wa watu, amemfungia safari kutoka Mombasa mpaka Unguja. Akimwoa kitakuwa chuo chake cha pili. Huyu mwingine bado mbichi, mwari, bikira, atakapomwoa itabidi arusi aijibishe mwenyewe. Arusi ijibu; yeye ajithibitishe urijali wake na mwenzake athibitishe ubikira wake.” (Vuta Nkuvute).
Je unataka kuwasiliana naye Shafi? Mwandikie barua pepe: ashafi40@yahoo.com
Ukitaka kitabu cha Haini kinauzwa duka la Longhorn karibu na Mfuko wa Utamaduni pale Kinondoni, Dar es Salaam, namba 1237. Simu zao mbili : 26-67334; Mobaili : 0748335702.
Soma msururu wa vitabu vyake vinavyopatikana na namna gani hapa:http://www.bookfinder.com/author/adam-shafi-adam/
duuuh… NIMEISOMA HII HABARI YA SHAFI NIMELEWA!!! KIFUPI NIMETAKA KUSAHAU KAMA MIMI SIKUWEPO KATIKATI YA WATU HAWA WAWILI. NILIJIHISI KAMA NA MIMI NILISHUHUDIA MAONGEZI YAO HAWA WAANDISHI WAWILI WALIO KAMA WAFALME KATIKA LUGHA NA UTAMADUNI WETU WATANZANIA. MUNGU AMPE UMRI MREFU MZEE WETU SHAFI PAMOJA NA RAFIKI YETU KIPENZI FREDDY MACHA. NIMEFURAHI SANA KUSOMA HABARI YA SHAFI, AFADHALI WENGI WETU WASIOMTAMBUA MZEE HUYU WATAPATA KUMTAMBUA.
Freddy,
Naona nina bahati,kama ile ya mtende,kuweza japo kusoma unyambulishi huu wa lugha na wa kumhusu huyu gwiji wa sanaa ya utunzi na uandishi,Shafi Adam Shafi. Hakika,kama ulivyosema,huyu ni kisima cha busara na historia za kule tutokako. Kule tunapowaza kurudi kila siku ingawa kila mara tunajikuta tupo njia panda.
Kitabu cha Kuli ndicho ambacho nakikumbuka zaidi.Kilinifanya nikalipenda somo la kiswahili kwa dhati. Bado ninakumbuka kilivyoisha kitabu kile “Yana mwisho haya”. Hali bado ni ile ile.Kilichobadilika ni rangi ya ngozi ya mtawala.
Shukrani za pekee kwa kutukumbusha kwamba Shafi bado yupo,bado anadai na muhimu zaidi bado anaandika.Tutamsoma na wenetu pia watamsoma.
Asante Freddy. Sio mara ya kwanza umetuandikia kuhusu Adam. Na bado nina hamu kusoma zaidi juu yake toka kwako. Ni vitabu vya watu kama yeye vilitufanya kupenda kujisomea, lugha, utunzi, n.k.
ahsante sana Freddy…inawezekana mi ni mmoja wa vijana ambao bado tuna uchu wa kujua mengi kuhusu lugha yetu ya Kiswahili, hususani fasihi andishi. Mi niliwahi kusoma Kuli zaidi ya mara 10, bado kinanipa muwashawasha wa kuendelea kukisoma..
Ningependa uendelee kuwaelimisha vijana hasa wa kizazi cha leo “Bongo Flava” umuhimu wa watu kama Shafi Adam Shafi.
Mungu ampe maisha marefu
hayo tu kwa leo
Fred, Habari za shughuli.. Nashukuru sana kwa habari.Hazina yetu bado haifichiki.Mzee wetu Adam bado anatukumbusa… Elimu kwa kusoma vitabu bado yawezekana kwa kiasi kikubwa.
Tudumishe usomaji wa vitabu kupata elimu hasa kwa wenye utunzi kama mzee adam
Ushiriki wako ni muhimu kwa kutupasha habari
Mungu ambariki mzee wetu
nimetokea kumkubali mzee shafii. nlipo soma kitabu chake cha vuta”nkuvute . ni miongoni mwa vitabu mashughili,
Sahihisho. Kitabu cha kwanza allichoandika Shafi si Kuli. Ni Kasri ya Mwinyi Fuad. Nina hakika. Nilikihariri na kukichapisha mimi.
Walter Bgoya.
Halafu, ni “saa nne” na ….” “Masaa manne”, na “lisaa limoja” ni uharibifu!!
wb
Sawa Kaka Bgoya, nimesahihisha Kiswahili (“masaa”) na kunyoosha wakati wa vitabu Kuli na Kasr vilipotolewa. Wasomaji wanaotathmini kama nyinyi ndiyo wajenzi wakubwa wa jamii zetu. Shukrani.
Hi Freddy.
that was fanastic ,Good job!! youre realy an author not an example of an author
Cheers
Angel
Fred habari ndugu yangu nimevutiwa sana na jinsi ulivyojitahidi kumpata Ustadh Adam Shaffi mpka ukaweza kutuhabarisha.Hata mimi nina tatizo la kutojua vema lugha yetu nimepata changamoto sana.
Kila kheri Fred
hi kazi ni bora
asante
nampa shavu mshikaji namkubali ile mbaya kweli anaiweza kazi
nampa shavu mshikaji namkubali ile mbaya kweli anaiweza kazi.si unajua tena wabongo/ tunabaniana sana big up SHAF hiyo kweli talent yako .hivi kuna mtoto wako aliyerithi mikoba ya kuandika andika?
Fredy safi sana, unajua mimi nilimuona kwa macho live hapa UDSM siku hiyo aliitwa na mwl wetu mwandishi mwenzie maarufu kama mzee wa NGOSWE,Edwin Semzaba ilikuwa mwezi wa sita mwaka huu 2009, kweli uliyoyaongea juu ya mzee mwandishi huyu uko right brother, hata hicho kitabu kipya alituambia habari zake.Nimesoma vitabu vyake takribani viwili[vuta nkuvute na kuli] na saivi nimenunua kitabu chake kingine cha Kasri ya Mwinyi Fuadi,kweli huyo mzee ni manju tena haswa,na hazina kubwa katika Fasihi ya Kiswahili
Freddy,
Nakupa hongera kwa kutuhabarisha mambo mazuri kama haya. Na vilevile kutukumbusha juu ya suala la kujisomea ili tuwe wabunifu kupitia makala au vitabu vya watu wengine. Mwili unanisisimka nahisi kama kuna mambo mengi ambayo yananipita lakini najipa moyo na kusema ,”yana mwisho haya” Asante sana.
KWA WAPENZI WA FASIHI YA KISWAHILI KAZI ZA SHAFI ZIWE CHANGAMOTO KWETU HASA KATIKA UANDISHI. VIJANA TUJIJENGEE TABIA YA KUWA WABUNIFU NA WENYE KUWIWA NA UKUZAJI WA FASIHI.SHAFI AMEANZA KUZEEKA SASA TUNAHITAJ WARITHI.
i came across your blog as i was browsing and i paused, i paused for a minute , then i continued to the very end.
wallahi sijawahi kusoma novel au kitabu cha kiswahili, sikumbuki.. labda nilivyokuwa skuli, kitabu cha shamba la wanyama na hivi sasa nikiulizwa kitabu chenyewe stori yake, sikudanganyi, sikumbuki kitu.
sikufikiria kama naweza kujipa nafasi ya kukaa na kusoma kiswahili mpaka baada ya kukumbana na blog yako. ama kweli mimi nimejitupa na kujisahau na kusahau umuhimu wa lugha yangu.
nimeanza kusoma novels hivi karibuni na nimevutiwa sana na vitabu na naamini hivi sasa zaidi ya wakati wote wangu kuwa elmu ni muhimu na kweli ni muangaza.
nimeagizia vitabu kutoka kenya na kuanza kusoma vitabu vya kiswahili na nashkuru kwasababu ni baada ya kupitia hii blog yako.
Naamini ya kuwa hata mimi naweza kuandika kitabu. Mungu ataniwezesha.
Shukrani
Kweli ungeanza kujifunza Kiswahili, maana lugha umeichanganya changanya na kuiboronya. KIswahili ni moja ya lugha kumi kuu zinazokua haraka duniani leo …iko ghorofa moja na Kispanyola, Kichina, Kiarabu, Kireno, nk.
kaka fred big up kwa kumtafuta babu yetu shafi kwani siku nyingi natamani kupata taarifa zake na nimezipa japo si sana nashukuru kwani mzee huyo amekua akinivutia na kazi zake nzuri za fasihi .Nilikuwa na swali kaka angu linasema kwamba nini chanzo kabisa cha fasihi wengine wanasema fasihi chimbuko lake ni mungu wengine wanasema ni mabadiliko ya binadamu nashindwa kupata jibu kamili kuhusu hili naomba unisaidie ili niweze kufanya kazi za kifasihi nikiwa najua chanzo kabisa cha fasihi.
nakutakia kazi njema…
Y-Dah,
(Hili jina la kweli au la utani?)
Nashukuru umeandika na kwamba unamhusudu mtu aliyepevuka kama gwiji, ustaadh Shafi.
Kuja katika swali lako….
Chanzo cha fasihi ni maongezi na lugha ya wanadamu.
Toka tulipoanza kuzungumza tumekuwa na fasihi simulizi. Hatimaye binadamu walipoanza kutumia maandishi kutangaza waliyoyasema (yaani hadithi, mashairi, sanaa za maonyesho na kisha sinema na leo video) fasihi imekuwa suala la lazima katika kufunza, kustarehesha na kuzijenga jamii mbalimbali za wanadamu.
Kila mtu ana mawazo yake kwa hiyo endelea kutafiti; hayo ndiyo maoni yangu kwa kifupi.
Leo nimekutana na mkwe wake oxford nikahisi kama vile niko naongea na mzee mwenyewe Shafi na ndo kisa cha kukimbilia kumgoogle nilivyotia mguu nyumbani kwani siamini macho yangu nilidhani mzee wetu keshachoka kwani wakati nikiwa shule nilikuwa nashindwa kufikiri kama ni mtu wa kawaida kabisa.Mungu amzidishie uhai dunia nzima inampenda.Wakati nikiwa shule sikutosheka na kitabu chake tafadhari anaeweza kusaidia jinsi ya kupata kitabu cha kuli naweza kununua ili ninoe akili.
Vitabu vya Adam Shafi vinapatikana duka la Soma Cafe pale Dar es Salaam. Je, umewahi kuisikia , iko mtaa wa Chato, si mbali na Kinondoni kuelekea Mwenge… Ikishindikana nenda duka la vitabu la Chuo Kikuu cha Mlimani; ama watafute wadau wa Mkuki na Nyota. Meneja mkuu aliwahi kutoa vitabu vyake Shafi miaka ya Sabini.
Tovuti yao ni http://www.mkukinanyota.com
kimsingi nikupongeze mdau kwa namna ulivyo tuunganisha na gwiji wa kiswahili SHAFI ADAM SHAFI ambaye na sisi tunajisifia kwa kazi zake kama walivyo wenzetu WA NIGERIA jinsi wanavyojivunia CHINUA ACHEBA,
nimefuatilia kwa kuzisoma kazi tatu za gwiji huyu ambazo ni (KULI, VUTA N’KUVUTE NA KASR YA MWINYI FUAD) nilipendezwa sana na kazi zake natamani sana kupata kazi yake ya HAINI ni namna gani naweza ipata maana nimetafuta kwenye maduka ya vitabu sijafanikiwa kuipata nadhani ni kulingana na maeneo ambayo nipo kimsingi ni maeneo ambayo watu hawana utaratibu wa kujisomea vitabu..
mdau siku nyingine ukipata saa nne au nyingine zaidi ya hizo uwe unatupatia machache kama si yote uliyomegewa na gwiji huyu
Ahsante Mahimbi…. kuhusu kitabu cha Haini au vingine nadhani huuzwa maduka machache sana…Afrika Mashariki. Pale Dar ni moja liko mtaa wa Kinondoni.
Labda mpigie tu simu mwenyewe Mzee Shafi umuulize : 07132-66560
Ukishampigia nieleze nijue kuwa umewasiliana naye.
Niandikie Email hapa : kilimanjaro1967@hotmail.com
asante kwa kuiendeleza fasihi kizazi hadi kizazi.
ASALAM ALAYKUM!
Nimesoma Kuli, Kasri ya Mwinyifuadi, Vuta ni Kuvute, Haini na unaposoma vitabu hivyo unakuja kufahamu kua Shafi ni mwanaharakati ambaye amejitolea maisha yake kutaka kuiona Zanzibar inakua sawa na Singapore, Taiwan, Porto Rico na kwengineko. Sahfi anakuonyesha Kuli alivyokua anafanya kazi na maisha yake ya shida, na akijua kuna siku atakuja kua huru.
Hadithi inapomalizika nikusema kua ni Mapinduzi tayari, sasa ona maisha yalivyokua na namna Rashidi alivyokua akitegemea, Sahfi mwanaharakati alichokisema kipo kwenye Haini, kafungwa kwa sababu ya kifo cha Kiongozi, lakini ukweli ndio wanadamu ilikua sawa kuwatesa wenzao na kuwatia vilema hadi leo? Shafi kati ya Vuta ni Kuvute ni yeye mwenyewe ndio aliyefika katika dimbwi la Huba la Yasmin, yeye ni mfuasi wa Umma Party ya Babu na unafahamu zaidi vitabu vyake ukiwa mzalia wa Zanzibar.
Nilikutana na Shafi mwaka wa 1999 akaniahadithia juu ya vitabu 2 vyake moja ni Mbali na Nyumbani na chengine Anakabili Mlima Elgon nikaja badae kujua vyote vilikua ni kitabu kimoja. Shafi ni damisi, lakini ukikaa na Shafi ukiona ile General Knowledge aliokua nayo ni kubwa kabisa na ndio unamuoana kama Professor Abdulrazaka Gurnah wa alioandika Doti, Memory Departure, By The Sea ni watru wa khulqa moja na ndio Wa-Zanzibari walivyokua, lakini mfumo wa elimu ukaja ukaparaganyika ndio kizazi kilichofwata unawakosa kina Gurnah, Shafi, Bwana MSA, Mohammed Said na wengineo.
Kiswahili kinahitajia kuandikwa na kina Sahafi kupewa nafasi ya kutoa vijarida.
Ama kweli na wewe Ben Rijal unalo jicho na upeo wa kuona umuhimu wa hawa wananafasihi na pia kulinganisha na jamii nyingine. Nakubaliana nawe kwamba Kiswahili kinahitajia kuandikwa kwa kina. Ila wapo waandishi wengine wazuri mathalan Profesa Said Ahmed Mohammed na Prof Farouk Topan nk wanaochapa vitabu vyao Kenya …ntawaletea mahojiano na gwiji Said Ahmed (aliyeingia na kitabu mashuhuri cha Asali Chungu mwaka 1977) karibuni. Huyu ni jabali jingine la Kiswahili na fasihi yetu adhimu toka visiwani.
JAMANI KUMBE SHAFI ADAM SHAFI bado yu hai? Asante Ndugu kwa kutujuza!
Wallahi namwenzi mno mzee huyu kwa kazi zake kuntu za fasihi. Twakutilia dua ya umri mrefu mzee wetu ili uzidi kutajirisha fasihi ya Mwafrika!
Du kwa kweli uandishi ni kipaji kikubwa sana na namkubali. Sana kwa kweli hasa kwa kazi yake ya vuta nkuvute
Ni bora kusema kidogo chenye kueleweka kuliko mengi yenye kuchosha
kaka Freddy, hongera sana naikumbuka sana kazi yake ya “vuta n’kuvute” ni kitabu kilichopendwa sana hususani pale sekondari ya jitegemee ni mwanafunzi yupi aliyesoma kiswahili kidato cha 5/6 pale, asivifahamu vitabu vya Shafi naamini hata kuwa kwangu Mzumbe nikisomea sheria Babu shafi amechangia maana kwenye NECTA nilitumiavitabu vyake.Sikujua kama mzee wetu yupo hai nami namwomba Mungu amzidishie uhai. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . ila pia kaka swali je,unawakumbuka na wanafasihi wengine kama akina Haji Gora Haji,Theobald Mvugi na n.k na kutupa taarifa zao au we unajihusisha tu na Mzee wetu Shafi.
Imani, ahsante kwa hoja. Ama kweli Mungu amzidishie mzee Shafi na wanafasihi wengine wanaojenga tunzi na tungo zetu Afrika Mashariki, nk.
Kuhusu swali lako mwishoni.
Kama unafuatilia makala zangu miaka mingi utagundua kwamba Adam Shafi siye mwandishi peke yake (au msanii maarufu) “ninayejishughulisha naye” kama unavyosema. Naomba kukuuliza. Je umenisoma toka lini?
kaka fredy nimekumbuka sana vuta nkuvute hasa harakati za denge na ukombozi, na yale mapenzi ya yasmini kwa denge… umenikumbusha nyuma sana nilipokua najifungia ndani na kusoma vitabu kama… kila kukicha
nimerudi tena baada ya ushauri ulionipatia wa namna ya kuipata kazi ya HAINI na nimefanikiwa kuipata labda ningependa kujua machache katika uandishi wa gwiji huyu hana muendelezo wa moja kwa moja wa kazi zake, mfano katika vuta n’kuvute hatujaiona hitma ya mwanaharakati kama denge ningeomba kama anamuendelezo wa kazi zake hizi tunahitaji kujua maisha haswaa baada ya uhuru , je serikali mpya ilizienzi harakati hizi… MACHA naomba uwasilishe kwenye dk 40 zingine za wewe na shafii
katika maisha yangu yote ya shule hakuna kitabu cha riwaya ya Kiswahili kilichonvutia na kukipenda kama Vuta N’kuvute. Mzee wetu ni mtu hodar sana na ana kipaji cha nguvu. Mwenyez mungu amzidishie kila la kher
moyo wangu hukupatwa kuathiriwa mpaka niliposoma vitabu vya shafi adam shafi ndipo nilipojigundua kuwa nami ni mwandishi mzuri. mwenye zimungu akulinde gwiji wetu
[…] Kuna taarifa ya mahojiano ya kina baina ya Shafi Adam Shafi na Freddy Macha ambayo unaweza kuyasoma hapa. […]
[…] Katika saa nne zote nlizokuwa naye ananikumbusha moja. Ikiwa umewahi kuvisoma vitabu vyake utagundua huchanganya kila kitu: furaha, simanzi, vita, amani, mapenzi, karaha, starehe, maonyo, mandhari, elimu na mengine tele. Ukiongea naye yuko hivyo hivyo. Mastore kibao. Anaelezea namna wachapishaji waliotafsiri moja ya vitabu vyake walivyotaka kumrusha fedha. Akawafungia safari hadi Paris kudai haki hiyo. Au alivyofiwa na mpenzi wake wa ujanani zamaaaani…pamoja na mtoto. Alivyotiwa jela ugenini ujanani (anamalizia kitabu kipya kuhusu kisa hiki, soma mbeleni); alivyofungwa Unguja baada ya mauaji ya Rais Karume. Hadi leo mguu wake wa kushoto ananionyesha bado una dosari (“pana ganzi pajani shauri ya kulala sakafuni”); alifungwa miaka miwili. Visa, kibao. Vyote vimepenyezwa angalau kiduchu ndani ya vitabu vyake. Vingine vishatafsiriwa lugha za kigeni. Kimoja kilishinda tuzo. Niko naye. Tunakula ubwabwa uliopikwa vizuri na binti yake kwa nyama za kukaanga…huku tukila huku tukiongea. Mazungumzo hayaishi. Ingawa masaa manne mengi kukaa na mtu (kwa huku Ulaya ambapo muda ni dhahabu) nahisi itabidi nipewe miezi ili kujua mengi zaidi ambayo nataka kuyafahamu. Anachonifurahisha ni hii picha akiwa na mjukuu wake wa miaka minne. Huyu ni mtu aliyeshaishi. Akaona mengi. Akazaa. Akalea. Aka…mcheki. Waandishi ni watazamaji na wasikilizaji wakubwa wa jamii. Waandishi ndiyo hutukumbusha yaliyotokea. Kusingekuwepo waandishi tusingefahamu yaliyopita. Kila mmoja wetu kila siku anahangaika na maisha. Tunaamka, tunakula, tunakwenda kazini au masomoni. Tunarudi , tunalala, kesho yake hayo hayo: kila kukicha na kuchwa tunaona mengi, tunayapita, tunayasahau. Ila waandishi? Wasanii? Kazi yao kuweka kumbukumbu ya haya mambo. Kuyahadithia. Wapo waandishi wa aina nyingi. Wana habari. Waandishi wa elimu na historia. Washairi. Watunzi wa muziki na nyimbo. Sinema. Tamthiliya.Wapo waandishi wa fasihi kama Adam Shafi. Shafi alianza na kitabu cha “Kuli”, kinachoelezea mgomo maarufu wa wafanyakazi maskini , Unguja mwaka 1948. Anasema alikuwa na miaka minane tu. Na ingawa anakumbuka juu juu tukio hilo utotoni, alikuja kuhaditihiwa na mtu akaweka kumbukumbu na baadaye maandishini. (Unaona waandishi walivyo watu muhimu, kutukumbusha?) “Kuli” kilichapishwa na Tanzania Publishing House (TPH) miaka ya Sabini. Lakini awali alichapisha “Kasr ya Mwinyi Fuad” ambacho kimeshatafsiriwa lugha tatu za kizungu: Kijerumani, Kifaransa na Kirusi. Miaka ya karibuni, Shafi kaibuka na “Vuta Nkuvute” kilichopata Tuzo kwenye tamasha la vitabu, Dar es Salaam, mwaka 1998. Ni kisa cha mapenzi, tena mapenzi makali na mazito kati ya msichana wa Kihindi na Mwafrika. Humo mna siasa na harakati za uhuru na mengi mengine. Mseto mkubwa wa mapenzi na siasa, ambao si waandishi wengi wa KIswahili wamemudu kuuchanganya. “Vuta Nkuvute” kilichapwa na Mkuki na Nyota. (Soma habari zao hapa : http://www.mkukinanyota.com) . Mwaka 2003 mwanafasihi huyu alitoka na “Haini” ambacho kama anavyosema mwenyewe kiliogopwa na wachapishaji wengi nchini. “Haini” si mchezo. Kitabu cha moto, cha kuchachafya. Soma ukurasa wa kutisha wa mfungwa mmoja akipambana na chatu, ukurasa wa 172: “Anaiangalia dunia kwa hofu na kukata tamaa, anachungulia kaburi. ..Alipomtazama yule chatu alimwona anaanza kujinyumbua, ananyeka, kichwa amekiinua,kama anayezindukana kutoka usingizini. Chakula chake amekwisha andaliwa, hana wasiwasi. Tayari kimo mle chumbani.” Kama desturi visa vyote vya Shafi hujaa mateso, shida, majonzi, taabu za Mwafrika; lakini haviishii na hisia hizi za kukata tamaa na kutokwa machozi. Wahusika wake huteseka lakini mara wakaibuka, wakaamka na kupambana na matatizo yao. Matumaini ndiyo rangi ya suluhisho lake. “…Moyo wa ujabali ukamjaa tele akahisi na nguvu kama za simba yuko tayari kuvaana na chatu yule kwa mikono yake miwili. Chatu naye amenyanyua kichwa anajiramba midomo. Huutoa ulimi wake halafu akaurudisha ndani na pale anapoutoa utadhani anatoa miali ya moto kutoka mdomoni. Wanatazamana. “Nani atakayeanza kushambulia?” Haramia anajuliza.” Msomaji sin’takueleza yaliishia wapi. Maana ukijua hutatamkiwa kitabuni. Nnachokumbuka sikulala baada ya kusoma sura hii. Inatisha. “Haini” ni kitabu kinachosisimua sana. Kilinikumbusha visa vya mwandishi wa Kimarekani Stephen King, ambaye karibu vitabu vyake vyote vishafanywa sinema. Sinema yake maarufu ni ile ya kutisha sana iitwayo The Shining. Sidhani ntakosea nikisema maandishi ya Shafi hayapishani na waandishi wa aina hii hata kidogo. Vikitafsiriwa vitapendwa ulimwenguni kote. “Haini” yahusu namna Shafi alivyofungwa jela miaka miwili akiwa bado mwandishi wa habari (taaluma yake kikazi)…akifanya kazi gazeti la “Uhuru” ambalo enzi za miaka ya Sabini (alipowekwa kizuizini) visiwani liliitwa “The Nationalist.” Ubaya,walakini, mmoja. Kitabu hiki kimechapishwa Kenya na Longhorn (http://www.longhornpublishers.com). Bongo hakipatikani kirahisi bali duka moja tu mitaa ya Kinondoni. Vitabu vyake vyote Shafi vinaonyesha maisha ya sasa na yale yaliyopita. Anapenda kuhusisha historia ya jamii. Kwa hivyo mbali na kustareheshwa unafahamishwa mambo yaliyopita ya zamani. Hali hiyo imo pia katika muswada wake mpya “Mbali na Nyumbani” ambao unaelekeza maisha ya ujanani wa mwandishi. Namsikiliza mwanafasihi huyu aliyezaliwa Unguja mwaka 1940 akinisomea: “Mbali Na Nyumbani.” Anasema huchukua wastani wa miaka mitano kumaliza kitabu kimoja. “Huwa sina haraka hata kidogo…” Huandika kwanza kwa mkono halafu ndiyo akachapa katika tarakilishi (kompyuta)….”Mbali na Nyumbani” anafafanua, kinasimulia ujana wake kati ya mwaka 1960 na 1967 …akijaribu kuvuka Afrika kwenda Ulaya. Hapa alipo ukurasa wa 427 (cheki picha juu)anasimulia akiwa mpakani Sudan kuingia Misri. Anaposoma ananikumbusha mwaka 1978 nilipojaribu na mimi kustoawei kwa meli. Vijana enzi hizo tulitaka sana kupanda meli. Ubaharia ulikuwa kazi ya kutamanika, kutafutwa na kuotea. Miaka hiyo imepita. Leo Vijana bado wanaotea kuingia nchi zilizoendelea. Nchi za Magharibi. Maisha yalikuwa magumu enzi zile, bado magumu leo, miaka arobaini na sita baada ya Uhuru. Lakini Wazungu wamefunga mipaka. Hawataki wageni. Enzi hizo ilikuwa vile vile. Kupata “kitabu”ilikuwa kazi; leo pia iko kazi. Kupata visa ilikuwa kazi; leo pia iko kazi. Miaka kumi na mitano iliyopita mtindo uliibuka kwa Mwafrika kujifanya mkimbizi. Hiyo ziku hizi imeshatafutiwa ufumbuzi. Wazungu washajua. Washajua mathalani kuwa Bongo hakuna vita. Yalipokuja mauaji na machafuko ya Burundi na Rwanda wengi tukaanza na sisi kujifanya wakimbizi kutoka sehemu hizo. Ujanja huo ulifaa hadi miaka michache iliyopita. Leo yamegeuka. Wahusika washagundua. Ukimbizi leo haufai tena kama sababu. Yuko jamaa kanieleza ujanja mpya. Kujifanya junya au firauni. Si mnajua tena kuwa jadi hii nchi za Kizungu inaruhusiwa? Mwanaume kuoa mwanaume au mwanamke kumwoa mwanamke mwenzako? Mwezi jana ilipitishwa sheria Uingereza kuwa ukishtakiwa kuwa umemtania msenge au firauni unakwenda jela miaka Saba. Vituo mbalimbali vya polisi vina vitengo maalum vya kutetea maslahi ya wasenge, na vinaongozwa pia na polisi wasenge. Basi kusikia hayo walala hoi nao wamegundua mpya. Afrika tabia hii hairuhusiwi wala si mila yetu. Basi ukitoka kwenu ukisema umeteswa kwa kuwa wewe msenge, ah unakaribishwa mikono miwili. “Kwani watakucheki?” anauliza mpambe aliyenieleza. “Watakucheki vipi? Watakufungua makalio?” Basi, ndoto na njozi za kutoka Afrika kwenda Majuu hazikuanza leo. Kitabu kipya cha Mzanzibari Shafi, kitaonyesha harakati hizo miaka ya zamani kabla wengi hatukuzaliwa. “Mbali na Nyumbani” anasema kimeshauliziwa na wachapishaji kadhaa hapa Bongo na Kenya. Pichani chini Adam Shafi akinisomea muswaada. Lakini swali niulize. Wangapi wanamfahamu Adam Shafi? Kwa wasomaji wa vitabu vya hadithi na fasihi, jina hili ni la kusisimua na kuvutia. Kwa wapenzi wa lugha yetu tukufu ya Kiswahili huyu ni mjumbe. Walii. Tarishi. Al Watan. Mpiganiaji. Mbunge wa lugha hii. Ndugu msomaji nikupe mfano? Hebu kumbuka Wabongo wangapi wanaodai eti hawana msamiati wa kutosha kujielezea Kiswahili. Utamsikia mtu kasoma, ana shahada, ana ujuzi na utaalam wa hali ya juu akisema : “Ah siwezi kuandika barua kwa Kiswahili…” Ilhali (lakini) anaongea Kiswahili fasaha lakini kuandika anashindwa. Anatumia Kiingereza. Kiingereza chenyewe marea nyingi kibovu. Afadhali hicho Kiingereza kingekuwa kizuri. Msikilize babu na gwiji wa fasihi ya Kiswahili, Ustaadh Shaaban Robert akituasa katika Utenzi wa Adili: “…Lugha humpa hadhi Kutumia ajuaye.” Kisa cha kusema haya yote nini? Ukitaka kuboresha lugha, ( yeyote ile) soma vitabu. Soma hadithi. Soma mashairi. Kama vile ambavyo wanamuziki hujiendeleza kwa kusikiliza miziki ya aina mbalimbali, msamiati, lahaja na lugha huendelezwa kwa kusoma vitabu. Kwako msomaji unayegomba huwezi kujieleza vizuri kwa Kiswahili, au kuandika Kiswahili…katafute vitabu vyake Adam Shafi, utafaidika na kustareheka. Watanzania tunasemwa hatusomi. Baa ziko nyingi kuliko maduka ya vitabu na maktaba. Taifa lenye watu wasiosoma linajichimbia kaburi la ujinga. Nikiwa na Shafi, mjini Milton Keynes alipopitia juma lililopita. Picha imepigwa na Hawa Yaxley. Hebu onja (kidogo) baadhi ya ubingwa wake wa matumizi ya lugha katika nukuu zifuatazo (hapa ni vitabu viwili tu): “Alihisi Shihab alikuwa kama aliyemtupia mshipi akaumeza pamoja na ndoana, chambo na chubwi.” (Vuta Nkuvute). “Aziz alitaka kuibusu midomo ya Khadija. Amemwinamia, uso umembadilika, uchu wa mwanamke umemtawala akili zake zimehama kutoka kichwa cha juu zimehamia kichwa cha chini. Alipotaka kumbusu Khadija alimtemea mate yakamtapakaa uso mzima. Alimwachia mkono mmoja ili ajipanguse yale mate, Khadija akaukamata mkono wake akaung’ata, Aziz akasikia maumivu makali yakipanda mpaka utosini.” (Haini). “Midomo aliitafuna tafuna nakuimungunyua mungunyua kama mtafuna tambuu…” (Vuta Nkuvute). “Tokea siku ile aliposokomekwa ndani mle, furaha kwake ilikuwa adimu na huzidi kugubikwa na majonzi pale anapowaza kwamba kosa alilolifanya ni kule kuchinja jogoo lake mwenyewe…” (Haini) “Amle Mbiza, amle Mboza? Aliwaona kama wote wawili wamemsimamia mbele ya macho yake, achague mmoja. Huyu mmoja keshaolewa, mke wa watu, amemfungia safari kutoka Mombasa mpaka Unguja. Akimwoa kitakuwa chuo chake cha pili. Huyu mwingine bado mbichi, mwari, bikira, atakapomwoa itabidi arusi aijibishe mwenyewe. Arusi ijibu; yeye ajithibitishe urijali wake na mwenzake athibitishe ubikira wake.” (Vuta Nkuvute). Je unataka kuwasiliana naye Shafi? Mwandikie barua pepe: ashafi40@yahoo.com CHANZO>>>> […]