Juisi la Mbuyu ndani ya kitabu cha Miriam Rose Kitunda.
Miriam Rose Kitunda (pichani chini) ni mpenzi mkubwa wa utamaduni wa Kitanzania. Na mapenzi yake hayaishii tu kwa maneno na bla bla.
Kwa miaka mingi amekuwa akiwasaidia Watanzania kughani na kuziremba tovuti na blogu zao bila malipo yoyote. Hii ni kwa sababu kasomea ufundi huu wa kisasa. Halafu amekuwa akitangaza mapishi ya Kitanzania ndani ya tovuti yake www.tasteoftanzania.com Mwaka huu anatazamiwa kutoa kitabu cha mapishi hayo ndani ya kitabu moto moto cha Kiingereza na Kiswahili.
Ukweli hadi sasa tunavyo vitabu viwili tu vilivyoandikwa na Watanzania kuhusu mapishi ya Kibongo. Cha kwanza kilitolewa na Eva Pendaeli Sarakikya (TPH, Dar es Salaam, 1977) na Zarina Jafrejji katoa mapishi ya Zanzibar ( Taste of Zanzibar, Gallery Publications, 2006). Vitabu ni hivi viwili tu vinavyofahamika, vilivyoandikwa na Watanzania. Kwa hiyo ni furaha kubwa kujua kiko kingine jikoni na mekoni.
Mtaalamu wa kodi toka PWC Tanzania, David Tarimo (kulia ) akijadiliana na Mwingereza aliyeishi Afrika Mashariki miaka mingi hata kuongea Kiswahili, John Small (katikati) na mshiriki mwingine. Picha na F Macha
Wawekezaji, wataalam na wafanyabiashara toka kona mbalimbali ulimwenguni wamekaribishwa kwa mkono wa kheri kuendeleza uchumi na maendeleo ya nchi yetu katika kipindi kinachofuatilia miaka 50 ya Uhuru.
Akiongea wakati wa Kongamano la Uwekezaji (“Tanzania Investment Forum 2011″) hoteli bab kubwa ya May Fair jijini London jana Ijumaa, Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa William Ngeleja alisema tuko katika kipindi kipya cha maendeleo ya uchumi chenye manufaa kwa wafanyabiashara. Waziri William Ngeleja akihutubia kongamano. Picha na Baraka Baraka wa Urban Pulse… Continue Reading »
Tamasha la kimataifa Ubongo Fest kuadhimisha maisha na kazi za mwanamuziki Remmy Ongala litafanyika mjini Dar es Salaam Jumamosi ijayo tarehe kumi, ukumbi wa Leaders, Kinondoni.
Tamasha hilo ambalo linaangukia sherehe za miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania litahusisha watumbuizaji toka Uingereza, bara Afrika na wanamuziki maarufu nchini mathalan Twanga Pepeta, Msondo Ngoma, Bendi ya Matimila, Jikhoman, Mrisho Mpoto na Banana Zoro. Aziza Ongala
Akifafanua habari hizo binti yake marehemu, Aziza Ongala, alisema Ubongo Fest inatukuza kazi za baba yake aliyeimba kuhusu umaskini, ulaji rushwa, maisha, imani, madhara ya UKIMWI na fahari ya Utanzania. Ingawa mwanamuziki huyu aliyebatizwa jina la “Dokta” na wanahabari, alizaliwa Kongo aliigeuza Tanzania kuwa nyumbani na familia yake baada ya kuhamia nchini mwaka 1978 akiimbia bendi ya Mzee Makassy.
“Ubongo Fest” alifafanua Aziza imetokana na neno Dokta Remmy alilotumia kufafanua mtindo wake wa “Bongo Beat” aliouimba na kwamba lengo lake ni kutumia tafrija kuwa jukwaa la wasanii wa kimataifa kuonyesha, kuvumbua na kutukuza vipaji mbalimbali vya watunzi nchini. Aziza na mumewe Mjamaika, Miael McGeachy wanaoishi London wanasema tamasha hili ni kipemgele cha Dk. Remmy Ongala Foundation iliyoundwa karibuni Uingereza kuendeleza kazi za Ramazani Mtoro Ongala. Moja ya matazamio yake ni kujenga shule ya wasanii na watoto yatima Tanzania.
“Lengo letu ni kutoa nafasi kwa wasanii wa Kitanzania kujenga mawasiliano ya kimataifa ili kusaidia ujenzi wa uchumi na utamaduni Tanzania. Ubongo Fest itakuwa mwanga mkubwa wa Kitanzania utakaorodheshwa katika sinema na rekodi. Ni mategemeo kujenga kiu ya soko la wageni kuja kwetu kadri tamasha litakapozidi kuimarika na kufahamika duniani,” wanaeleza. Miael McGeachy mumewe Aziza Ongala akiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Watanzania Uingereza, Said Surur(wa tatu kulia) na mdau wa Kitoto, mjini London kabla ya kuelekea Dar es Salaam kutayarisha shughul ya Ubongo Fest na mkewe na familia ya marehemu Ongala. Picha na Urban Pulse
Soma habari zaidi : http://www.dkremmyongalafoundation.com
Bongo ya joto, Bongo yenye kiu cha kujifunza na kujiendeleza.
Vijana walioparamia warsha chache nlizofanya Fasdo, Tandika, Dar es Salaam, Oktoba 2011 walikuja na maswali kem kem.
Walikuwepo washairi chipukizi wenye moyo na kujituma mathalan mwandishi Konisaga aliyesafiri toka Shinyanga kujua ataiendelezaje fani yake. Kati ya Watanzania waliodamka na kuazimia kujijenga ni Mshairi Konisaga toka Shinyanga.
Walikuwepo watengeza sinema wabichi waliokuja kuduhushi wakitaka kuiendeleza fani hii inayoanza kuwaka na kukua Bongo.
Taswira za arsha hii ya siku mbili zilikamatwa na mpiga picha kijana anayejituma, anayehangaika, anayejitaidi, kujiendeleza, Tikyomo Stephen Chande (chini, kushoto) akinikabidhi kinywaji kitukufu yaani Madafu…
Wacheza mpira pia waliwaka na kujitupa, kama yule aliyesumbuliwa na tatizo la musuli.
Au mzee mwenzangu, mtu wa makamo aliyesaidiana nami kuwatitimua vijana mazoezini siku jua lilipokuwa likiwaka utadhani tunachemshwa.
Wanawake walikuwa wachache lakini waliohudhuria walikuwa na maswali MAZITO.
Walikuwepo Watanzania wa kila namna, kabila na jinsia…na suala la unyanyasaji wa Ma Albino pia liliongelewa.
Swali mlima, swali simba, swali ugali, swali kuu la hizi warsha zote lilihusu maisha ya Ughaibuni.
Lakini sidhani Watanzania wanataka kuishi Ughaibuni. Wanachotafuta ni maisha bora. Ughaibu ina maana Uzunguni. Mazingira yanayosemekana yana ahueni, pesa, elimu, taaluma. Neno Majuu ni kigezo tu, chamb, ndoana.
Vijana wakiulizia je kazi zinapatikana Ughaibuni?
Je wafadhili wapo? Gumzo kuhusu ufundi mitambo na matumizi ya zana za sauti na muziki…
Na hata siku mvua iliponyesha Tandika bado wapo waliodamkia, waliopambana na Dala Dala, miguu au hata teksi kuchimba, kufukua, kuulizia, kudadisi na kunusa harufu.
Ukweli kuishi Majuu hakuna maana majawabu KAMILI.
Nchi yetu ina kila riziki. Ndizi kisukari si tu ngumu kupatikana Majuu; aghali ajabu… Maelezo kuhusu umuhimu wa mazoezi…
nchi yetu tajiri, nchi yetu imejaza kila aina ya rasilmali. Kinachohitajika ni watu wetu kuzidi kujipenda; na wale wenye taaluma nje na ndani kusaidiana kuichanusha Bongo yetu tamu na chungu kama asali na ndulele. Mazoezi ya tamthiliya na uso…
Utajipendaje kama hujifahamu?
Kwanza kijue ulicho nacho: Kiswahili na ngoma zetu za Sindimba na Bugogobo. Tuuafiki uzuri wa mazingira yetu; kupitia milima Meru, Njombe, Usambara, Pare, Uluguru, Nguru, Kilimanjaro, Oldonyo Sambo…tuzitambue nyika, nyasi, miti, maziwa na mito, Rufiji, Wami, Mbu, Pangani, Victoria, Tanganyika; bahari ya Hindi, visiwa vya Mafia, Pemba; nyika zenye wanyama pori wanaovutia kila aina ya watalii…
Tanzania yenye riziki…tamaduni na Kiswahili…
Je tufanyeje kukidumisha na kukiendeleza Kiswahili chetu?
Je, Kiswahili kina faida gani?
Vipi wenzetu Waingereza wameifanya lugha yao kuwa dhahabu, wanja na manukato ya ajira yao? Kwanza wametambua uzito na thamani ya lugha hii. Wanaendelea kuwatukuza waandishi wao, akina William Shakespeare na mwanariwaya Charles Dickens. Waingereza wanaitukuza lugha yao kiasi ambacho wamekuwa wavivu (ingawa si wote) kujifunza lugha za wenzao. Sisi wengine (na wenzao) ndo tunaopigania kujifunza kimombo. Hadi kujidunisha wenyewe… Watalii katika boti la Zanzibar wakijitahidi kupiga picha. Nchi yetu inapendwa kwel kweli.
Picha na mdau wa Kitoto…
Kwanini sisi wenyewe tukubali idunishwe?Kiswahili chetu si lugha ya kabila moja. Kiswahili chetu kinaweza kuwa ajira, kinaweza kuwa hazina, kinaweza kuwa ufunuo wa njia zilizozibwa.
Watanzania lazima tusome riwaya na fasihi zetu tuandike na tutukuze wasanii wanaokiimba Kiswahili kwa Bongo Fleva, Taarabu au hata nyimbo za dini.
Hilo lilikuwa moja ya gumzo kuu la semina hizi.
Kulizungumziwa pia suala la kufahamu taaluma ya elimu viwanda, sayansi na teknolojia. Vijana wa Fasdo waliulizia namna ya kuendesha mitambo ya kuendeshea muziki, sinema na maonyesho ya jukwaa.
Ujuzi dhoofu na finyu wa mitambo ni sayansi inayozifanya kazi zetu Waafrika kutoonekana maridadi. Kumbe safi kabisa na zina uwezo na hatima ya kupendeza na kutukuka ndani ya sayari yetu…
… sisi Waafrika wazuri wa sura, wazuri wa mandhari, tumeiva kwa visa na maisha kama walivyowenzetu wengine ulimwenguni.
Kutokana na taaluma dhaifu iliyoko katika picha na taswira zinazoonyeshwa katika sinema, muziki na kazi nyingine tunaonekana dhaifu.
Kumbe sivyo.
Sayansi hii iliongelewa pia. Nawashukuru Chande Nabora, mwanae, Tikyomo, dadake Lilian Nabora na mkewe Chande aliyetupikia misosi siku hizo mbili…
Warsha la Mei 2009, katika ukumbi wa British Council, Dar es Salaam. Picha na Innocent Swai
Kwa watakaohudhuria warsha za siku mbili ukumbi wa Fasdo, Tandika, mnaombwa mujisajili na Mkurugenzi Chande na mwenzake Nassib shauri ya masuala ya chakula na vinywaji.
Fasdo: (Faru Arts Development Organisation)
www.fasdotz.org
Chande Nabora: Simu 0713-310755
Nasibb: 0713-261011
Timu ya mpira ya vijana wa Fasdo. Picha na Lilian Nabora
R A T I B A
1.Jumanne 11 Oktoba, 2011…
Asubuhi ( saa tatu kuendelea)
Utangulizi: Kujuana na kusalimiana
Mazoezi ya viungo na kujinyoosha nyoosha
Mada : Afya na umuhimu wa mazoezi
Chakula cha mchana
Mchana (saba/nane)
Kujiendeleza : Umuhimu wa kusoma, kujituma, Fasihi na Lugha ya Kiswahili/ Kiingereza
Maswali na Majibu toka Wahudhuriaji
MUZIKI kwa wote (“jam session”)
Mdau wa Kitoto akicheza na mcheza dansa toka Nigeria, Funmi Adenkule, wakati wa tamasha la muziki wa Kiafrika lililofungwa na bendi maarufu ya Osibisa, London, 2004… Picha na Louisa Le Marchand…2.
Jumatano 12 Oktoba, 2011…
Asubuhi ( saa tatu kuendelea)
Utangulizi: Kujuana na kusalimiana
Mazoezi ya viungo na kujinyoosha nyoosha (kifupi)
Mada : Muziki na Kuimba
Mazungumzo kuhusu Muziki wa Tanzania unavyoendelea na matazamio
Chakula cha mchana
Mchana
Mada : Kujiendeleza / Maisha Ughaibuni
Uandishi na Fasihi : Umuhimu wake
Maswali na Majibu toka Wahudhuriaji
MUZIKI kwa wote (jam session)
VIFAA
1. Njoo na kijitabu cha kuandika, au chombo cha muziki kama mpigaji
2. Vaa mavazi rahisi kufanyia mazoezi na kanga, mkeka au kitambaa cha kutandika chini…
Mwana Kitoto akitumbuiza muziki wa “Berimbau” kwa kadamnasi na Sabu, mwalimu wa mchezo wa Kibrazili, Capoeira, mjini London, mwaka 2009. Picha na Louisa Le Marchand…
Mdau wa Kitoto natazamia kufanya semina mbalimbali za afya, mazoezi ya viungo, muziki, fasihi, lugha nk katika ukumbi wa Fasdo ulioko Tandika, Dar es Salaam; Jumanne tarehe 11 na Jumatano tarehe 12 Oktoba, 2011.Wote mnakaribishwa…
Moja ya shughuli lukuki zinazofanywa na kituo hiki cha maendeleo ya sanaa na michezo ni utengenezaji wa vitambaa vya Batik, vilivyofanywa na akina mama wa Fasdo. Picha na Lilian Nabora
Kiingilio bure.
Habari zaidi wasiliana na Chande Nabora, Mkurugenzi wa Fasdo. Simu namba 0713-310-755 au Nasibb 0713-261011.
Darasa la utengenezaji wa sabuni…. Picha na Lilian Nabora na Ticky Tedvan.
Tembelea tovuti yao : http://www.fasdotz.com
Darasa la kuimba. Picha na Lilian Nabora
Mfano wa warsha za mazoezi na afya ya mwili mdau niliyofanya Nyumba ya Sanaa mwaka 2009. Picha na Innocent Swai.
Nilitunga “Paka Mweusi” nikiishi Mwananyamala Kisiwani, Dar es Salaam…
1.
Paka Mweusi
Aligongwa na Gari
Barabarani
Saa za Jioni
Dereva akasema huo ni mkosi..
2.
Paka Mweusi
Alifia darini
Alikuwa akinuka
Nikapanda kumtoa
Nikaambiwa huyo ni jini…
3.
Paka paka jama
Kiumbe mzuri
Amegeuzwa
Kuwa ni shetani
Pale nilipopangisha nyumba ulilala uwanja wa mpira (wa mchanga) kwa nyuma na mbele ilisimama dede, baa kuu maarufu sana mtaa mzima wa Mwananyamala yaani, Wami. Jumba kubwa nililoishi lililokuwa na wapangaji na familia zaidi ya 10…lilikaa mithili wa taya kuu la kutokea “Mwananyamala A” kwenda Mwananyamala Kisiwani. Hapakumalizika vituko, mapenzi, ukahaba, masihara, uporaji, ukabaji, maisha ya watu waliofurahiana, waliozozana, waliotaniana, waliohusudiana, waliokosana; watoto waliocheza ndani ya maji, mchanga na matope; walionipa uelewa mkubwa wa jamii ya Waswahili na makabila mbalimbali jijini, Dar es Salaam. Mara moja moja utawaona watoto wadogo wakimbeba paka aliyeogofya wakamshika mkia kama tiara au pia wakamzungusha hewani, wakamrusha matopeni, mtini au juu ya paa ama ukuta utadhani kifuu cha nazi…
Nilihamia pale 1975 baada ya kumaliza jeshi; nikaanza kazi magazeti ya Uhuru 1976, hadi nilipohama mwaka 1982. Nikiwa jeshini Mafinga, Iringa, 1975…
1979 nilipotunga kibao hiki ulikuwa mwaka mgumu sana Bongo na Afrika Mashariki. Ndio mwaka majeshi ya Tanzania yalivyosaidiana na wananchi wa Uganda kumtoa kiongozi wao mnyanyasaji na muuaji, Idi Amin Dada; zikaanza foleni za vyakula na bidhaa muhimu. Mfalme Jean Bedel Bokassa aliyeangushwa 1979 akashtakiwa na watu wake kwa hatia za mauaji na udhalilishaji wa umma..
Kiulimwengu, ulikuwa mwaka wa viongozi wengi wakorofi sana kuangushwa mathalan, Rais Jean Bedel Bokassa wa Jamhuri ya Kati na Fransisco Nguema wa Equatorial Guinea. Ulikuwa pia mwaka ambao kilele cha mapigano ya Uhuru wa Zimbabwe…kilifikia…nikapata habari rafiki yangu mpigania Uhuru, Soul Zuka, kafariki akipigana na wenzake walioongozwa na Robert Mugabe na marehem Joshua Nkomo. Leo sijui Soul Zuka angesemaje angeiona Zimbabwe iliyopawatia uhuru Waafrika mwaka 1980…na aliyoimwagia damu..!
1979…vile vile ndipo wasanii wenzangu kadhaa walipoanza kuongelea kuunda bendi iliyokuja kuitwa Sayari. Mazungumzo yalifikia kilele Septemba 1981 tulipofanya onyesho la kwanza ukumbi wa Utamaduni wa Wajerumani, Goethe Institut…
Baada ya muda “Paka Mweusi” ulikuwa mmoja ya nyimbo nilizoimba na Wanasayari…
Nlikuwa nkiongea na Mkenya mmoja rafkiangu nkamuuliza : “Vipi ubalozi wenu unaweza kualika wadau kuja kufuturu?”
Jamaa ni mzawa wa Mombasa kwa hiyo Kiswahili chake mbolea kabisa. “Nyoooo!” Akajibu, “haiwezi kutokea.”
Watanzania tumebarikiwa kwa hilo.
Afisa Ubalozi, Carol Chipeta (kulia) akiwa na mwanamitindo na mablogi, Jestina George. Ulikuwa usiku wa rangi rangi, makutano na manukato. Picha ya Urban Pulse.
Mara ya kwanza kuulizwa kama mimi Mwislamu baada ya kumsalimia mtu “Asalaam Aleikum” ilikuwa hapa Ulaya. Salamu hizi za amani ni jambo la kawaida kabisa Tanzania; hazibagui kama huku Majuu.
Frank Eyembe wa Urban Pulse akiwa na binti yake mwanamuziki Remmy Ongala, aliyehudhuria futari na mumewe Miael toka Jamaika. Aziza Ongala na Miael wameanzisha shirika la kujenga kumbukumbu za kazi yake marehem Onagala (aliyefariki Desemba 2010). Wataanza kwa kishindo mwisho wa mwaka nyumbani. Bonge la maonyesho ya muziki jijini Dar es Salaam. Habari zaidi bofya Picha na Freddy Macha…
Nlikuwa usiku huo wa Jumamosi nimekaa mkekani na Mbongo mmmoja.
Akasema: “Haya mambo yalianzishwa na Mwalimu Nyerere. Enzi zake hakuruhusu kabisa mizozo ya kidini na uhasama na Waislamu kama ilivyo huku Ulaya. Miaka yote tumeishi kwa amani katika masuala ya kidini.” Afisa Ubalozi, I. Zahrani akiwakaribisha wadau kabla ya sala iliyoongozwa na Sheikh Mohammed Nassor.Picha na Urban Pulse.
Mambo hayakuwa mabaya kabisa. Pamoja na sala, maongezi na malaji; kwa mara nyingine tulidhihirishiwa namna uongozi mpya wa Ubalozini Uingereza unavyojitahidi kuwa karibu na watu.
Hebu tazama na sikiliza video hili lililotengenezwa kwa ushirikiano baina ya Urban Pulse na mdau wa Kitoto.
Leo nimepokea barua toka kwa mtaalamu wa jamii, habari, lugha na mpenzi wa nchi yetu, mwanae mhadhiri na msomi maarufu aliyefariki mwaka 2006, Profesa Chachage S. Chachage. Prof Chachage, picha ihsani ya Blog laIsae
Kama marehemu baba yake, kila ninaposoma au kupokea maandishi yake,Chambi Chachage,… hufarijika. Mbali na mada muhimu anayoiongelea napenda alivyotafsiri maneno “magumu” ya kitaaluma toka Kiingereza kuja Kiswahili fasaha. Jambo hili ni muhimu ukizingatia Wabongo wengi (na Wakenya pia) tunaosema eti maneno ya Kiingereza hayana tafsiri ya Kiswahili. Tunatukuza Uswanglish badala ya lugha fasaha. Ebo! Hebu msomeni: Ndugu Mwanazuoni Unayehusika Na Mada Hii,
Salaam za Saba Saba!
Katika ngazi ya Shahada ya Uzamivu (PhD) hasa kwenye Sayansi za Jamii (Social Sciences and Humanities) kilicho muhimu zaidi ni utafiti (research) ambao mwanafunzi ataufanya na tasnifu (thesis/dissertation) atakayoiandika. Hivyo sio lazima (sana) mtu awe kwenye fani fulani hasa kama hana mpango wa kuwa mkufunzi/profesa wa fani hiyo. Kwa mfano, ukifanya PhD hapa huwa unaruhusiwa kuchukua kozi kutoka kwenye idara/shule mbalimbali ili mradi tu uwe umechukua kozi za kutosha kutoka kwenye idara yako iliyohusika katika udahili (admission) wako chuoni. Hivyo, mimi mathalan nitachukua kozi za afya kutoka kwenye Shule ya Afya ya Jamii (School of Public Health), utawala kutoka kwenye Shule ya Tawala (School of Government), Sayansi ya Siasa, Fasihi, Stadi za Utamaduni na Jinsia, Historia, Saikolojia, Sosholojia, Anthropolojia n.k.
ila nikiwa nimelenga katika kufanya utafiti unaohusu masuala ya Afrika (African Studies) ambayo ndiyo fani yangu kuu niliyoifanyia shahada ya uzamili. Mpango wangu (ambao natumai hautabadilika kutokana na kuvutiwa na masuala/mada nyingi na hivyo kukosa mwelekeo(focus)) ni kufanya utafiti kuhusu namna ‘wasifu’ (identity) kama vile wa kimbari/kikabila/kiraia, kisiasa, kitabaka na kidini kwenye jamii unavyojengeka, unavyojikita na unavyobadilika katika – na kwa kutegemeana/kuendana na – muktadha wa migogoro anuwai juu ya rasilimali (natural resources).
Hapa PhD inasomwa kwa kufanya kozi kwa muda kisha ndio unaandika tasnia, ni tofauti na Uingereza na Tanzania (japo nilisikia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilikuwa katika mchakatao wa kuanzisha utaratibu kama wa Marekani ambao tayari Profesa Mamdani ameuanzisha kwenye Taasisi ya Tafiti za Kijamii Katika Chuo Kikuu cha Makerere (MISR)). Katika suala zima la kutuma maombi ya kupata udahili na skolashipu kilicho muhimu zaidi ni kulenga programu ya PhD yenye masuala yanayokugusa zaidi i.e. unayopenda na unayoweza kuyasemea. Natumai maelezo haya yatakusaidia katika harakati zako za kutafuta elimu na shahada pia.
Moja ya jambo kubwa sana ulimwengu wa sasa ni kuyajali na kuyahifadhi mazingira. Ukiutazama mji wa Dar es Salaam ulivyoharibika leo kutokana na 1. Msongamano wa magari 2. Mioshi na vumbi inayotakana na magari, mashine na barabara mbaya 4. Kutupa taka ovyo (hasa mifuko ya plastiki na chupa) kila mahali 4. Mpangilio mbaya wa ujenzi wa nyumba…
Utagundua kuwa mji umeshapoteza wajihi wake wa zamani. Jina asilia la Dar es Salaam lina maana “Bandari ya Salama” ; je usalama bado upo? Na je kama unafifia tutauokoa vipi? Mwana Kitoto nikiwa eneo la Tangi Bovu mwaka 2009; hapa karibu walikuwa watoto wakicheza, maduka na makazi …kila mtu pale mstaarabu, muungwana lakini mazingira yakiumia. Picha na Innocent Swai. Continue Reading »